SUDANI KUSINI

Juba: Hakutakuwa na maadhimisho ya Uhuru mwaka huu

Mmoja wa wananchi wa Sudan Kusini akipepea bendera kwenye sherehe za uhuru wa taifa hilo.
Mmoja wa wananchi wa Sudan Kusini akipepea bendera kwenye sherehe za uhuru wa taifa hilo. UN

Taifa jipya kabisa duniani, Sudani Kusini, imetangaza kuahirisha maadhimisho ya sherehe za uhuru, wakati huu nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya maelfu ya raia wake na kuharibu uchumi wake.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa habari na msemaji wa Serikali, Michael Makuei, amethibitisha Serikali yao kufuta sherehe za mwaka huu, kwa kile alichosema kuwa, kwa sasa nchi hiyo haiko tayari kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye sherehe na kwamba wanapaswa kutumia kiasi kidogo walichonacho kutatua shida za nchi hiyo.

Miaka iliyopita licha ya kugubikwa na tuhuma dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu na vita kwenye maeneo mengi ya nchi, Serikali ya Juba, ilikuwa ikiadhimisha sherehe za uhuru kwa kufanya magawaride na tafrija mbalimbali.

Maadhimisho ya uhuru wa Sudan Kusini hufanyika kila tarehe 9 ya mwezi Julai, na mwaka huu kwa mara ya kwanza toka ipate uhuru wake, hakutakuwa na sherehe zozote.

Katika hatua nyingine utawala wa Juba unakosoa hatua ya nchi za wafadhili kwa nchi hiyo kwa kukwamisha maendeleo yake kutokana na kuchelewesha kwa makusudi kutoa msaada wa fedha kuisaidia nchi hiyo.

Juba inasema kuwa masuala nyeti ya kutekelezwa kwenye mkataba wa amani uliotiwa saini na wakuu wa nchi hiyo, yanashindwa kutekelezwa kutokana na kukosekana kwa fedha.

Waziri wa habari wa nchi hiyo amesema kuwa, suala la usalama ambalo lilipewa kipaumbele kwenye mkataba wa amani, linashindwa kufikiwa kikamilifu kwakuwa hali ya usalama kwenye maeneo mengi ya nchi bado ni tete, na kwamba kukosekana kwa fedha za wafadhili kusaidia kutimiza lengo la kuimarisha usalama ni kikwazo kwao.