Maadhimisho ya Uhuru: Joseph Kabila awasili Kindu

Rais wa DR Congo, Joseph Kabila, akiwasili katika mji mkuu wa jimbo la zamani la Katanga, Lubumbashi, Juni 13, 2016.
Rais wa DR Congo, Joseph Kabila, akiwasili katika mji mkuu wa jimbo la zamani la Katanga, Lubumbashi, Juni 13, 2016. REUTERS/Kenny Katombe

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila, amewasili Jumatano hii jioni, Juni 29 katika mji wa Kindu, Maniema, ambapo kumepangwa Alhamisi hii sherehe ya maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Vikosi vya usalama vimetumwa katika maeneo mbalimbali ya mji. Katika uwanja wa ndege wa Kindu, ulinzi umeimarishwa na abiria wanakaguliwa vya kutosha.

Katika mji wa Kindu, watu wengi wanaonekana pembezoni mwa barabara kuu mbalimbali, wakiwa wamevaa nguo zenye rangi za bendera ya taifa au za vyama vyao vya kisiasa.

Mabango na fulana zenye picha ya rais Joseph Kabila vinaonekana katika mitaa mbalimbali ya mji. Majengo makubwa yamekarabatiwa na kupakwa rangi mpya.

Baadhi ya wakazi wanasema kufurahishwa na maandalizi ya sherehe ya kitaifa katika mji wa Kindu, kwa kuadhimisha miaka 56 ya uhuru mbele ya rais Joseph Kabila.

Mawaziri kadhaa wamewasili katika mji wa Kindu kabla ya kuwasili kwa rais Kablia. Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Mawasiliano na Waziri wa Afya ni miongoni mwa Mawaziri hao.

Matamasha mbalimbali ya muziki yamepangwa kwa kuwaliza wananchi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru.

Wasanii kama Werrason na Adolphe Dominguez watawaburudisha wananchi katika sherehe hiyo ya kitaifa.

Julien Paluku Walikale

Katika mkoa wa Kivu Kaskazini, maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru yatafanyika katika wilaya ya Walikale. Mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Julien Paluku, tayari amewasili wilayani Walikale tangu Jumanne hii, Juni 28, akiambatana na serikali yake ya kimkoa.

Kwa upande wa wakazi wa wilaya ya Walikale, kuchaguliwa kwa wilaya yao kwa ajili ya sherehe hii ni ishara ya heshima, hadhi na heshima kwa ajili yao.