SADC-LESOTHO

SADC yaipa Lesotho hadi Agosti kutekeleza mapendekezo ya tume

Waziri mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane.
Waziri mkuu wa Lesotho, Thomas Thabane. REUTERS/Siphiwe Sibeko

Nchi wanachama za jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, SADC, wameipa nchi ya Lesotho, muda wa hadi kufikia mwezi August mwaka huu, kuwa imetekeleza mapendekezo ya kurejesha utulivu kwenye taifa hilo la kifalme.

Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Lesotho hadi sasa haijatekeleza mapendekezo ya tume ya SADC iliyokuwa imeundwa kuchunguza mambo yaliyosababisha aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo, Tom Thabane kukimbia nchi yake miaka miwili iliyopita.

Akizungumza mara baada ya kutamatika kwa kikao cha wakuu wa nchi za SADC, rais wa Afrika Kusini, Jackob Zuma, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, anaimani kubwa kuwa, utawala wa Lesotho utafanya jambo sahihi.

Wakuu wa nchi za SADC wameendelea kuishinikiza Serikali ya Lesotho kutekeleza mapendekezo ya wakuu wa nchi kwa mustakabali wa taifa hilo ambalo limeendelea kushuhudia sintofahamu ya kisiasa licha ya kuwa na Serikali kwa wakati huu.

Baadhi ya mapendekezo mengine yaliyomo kwenye ripoti ya tume iliyokuwa imeundwa na SADC, ni pamoja na kuchukuliwa hatua ikiwemo kufunguliwa mashtaka kwa baadhi ya wanasiasa na wakuu wa jeshi la polisi waliohusika na mauaji na mkuu wa jeshi la Polisi nchini humo wakati wa jaribio la mapinduzi.

Nchi za SADC zimeendelea kuweka shinikizo la Lesotho na hata kutishia kuiwekea vikwazo na kuisimamisha kwa muda uanachama wake, lakini bado juhudi zake hazijafua dafu kwa utawala wa Lesotho unaosema masuala yake ya ndano hayaingiliwi na jumuiya hiyo.