COTE D'IVOIRE-SIMONE GBAGBO

Simone Gbagbo ashtumiwa kuchochea machafuko

Simone Gbagbo wakati kesi yake ikisikilizwa Juni 1, 2016.
Simone Gbagbo wakati kesi yake ikisikilizwa Juni 1, 2016. ISSOUF SANOGO / AFP

Kauli kali dhidi ya Simone Gbagbo, mke wa rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo, ilitolewa Jumanne hii Juni 28 na shahidi mmoja aliyetoa ushuhuda wake kwa machafuko yaliyotokea nchini Cote d'Ivoire mwaka 2010 na 2011.

Matangazo ya kibiashara

Ni kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa kesi ya mke wa rais Laurent Gbagbo, anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, kuonekana shahidi akimshtumu kufadhili na kuchochea mchafuko yaliyosababisha vifo vya watu wengi nchini humo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa zamani wa wanamgambo, Simone Gbagbo alichangia kwa kiwango kikubwa katika machafuko hayo kwa na kufadhili makundi ya watu wenye silaha.

Kiongozi huyo wa zamani wa wanamgambo, ambaye anajulikana kwa jina la utani "Kanali H," alijitambulisha kama kiongozi wa zamani wa kundi la wanamgambo, waliokua upande wa utawala wa Laurent Gbagbo. Kwa sasa anazuiliwa jela alifikishwa mahakamani akiwa amefungwa pingu mikononi.

Mbele ya majaji, na akiwa karibu na mke wa rais wa zamani wa Cote d'Ivoire, Laurent Gbagbo, Moise Metch alisema: "Ndiyo, wakati wa machafuko, tulipewa silaha, ndiyo, jukumu letu lilikuwa kutetea Gbagbo. Tulihusika katika machafuko hayo, hasa dhidi ya waandamanaji, ambao ni wafuasi wa Ouattara. "

Kisha alimtuhumu: "Simone Gbagbo alikuwa akitufadhili. Alikua mfadhili wa makundi ya wanamgambo waliojulikana kwa jina la Patriotes (wazalendo)" , makundi ya vijana, wafuasi wa rais wa zamani Laurent Gbagbo.

Ni kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa kesi hiyo, ambapo mke wa rais wa zamani wa Cote d'Ivoire anawekwa matatani kwa kuhusika kwake katika machafuko ya baada ya uchaguzi.

Hata hivyo tangu kuanza kwa kesi hiyo, Simone Gbagbo anendelea kukataa kuhusika kwake katika machafuko yaliyotokea mwaka 2010 na 2011.