DRC-KABILA

Miaka 56 ya Uhuru, Kabila asema, hakuna kitakachozuia uchaguzi

Rais wa DRC, Josephu Kabila, ambaye amesema hakuna kitakachozuia kufanyika kwa uchaguzi
Rais wa DRC, Josephu Kabila, ambaye amesema hakuna kitakachozuia kufanyika kwa uchaguzi DR

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Josephu Kabila, amesema Serikal yake iko tayari kwa mazungumzo ya kitaifa yatakayoshirikisha pande zote, na kutoa wito kwa wanasasa wa nchi hiyo kuheshimu katiba wanapodai haki yao.

Matangazo ya kibiashara

Rais Kabila amesema haya kwenye hotuba yake aliyoitoa usiku wa kuamkia leo wakati huu nchi hiyo ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 56 ya uhuru wa taifa hilo kutoka kwa Wabelgiji.

Rais Kabila, amesema hakuna njia ya mkato ambayo nchi yake inaweza kupitia kufikia suluhu ya kisiasa, na kwamba mapendekezo yaliyotolewa na mpatanishi aliyeteuliwa na umoja wa Afrika, Edem Kodjo, hakuna anayeweza kuyageuza ambapo amemtaka mpatanishi huyo kuharakisha kuanza kwa mchakato wa mazungumzo.

Kabila pia aligusia kuhusu matayarisho ya kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika mwaka huu, ambapo akawakumbusha wanasiasa nia yake aliyoonesha mwaka jana ya kuitisha mazungumzo ya kitaifa yaliyolenga kutathmini na kukubaliana namna bora ya kuandaa uchaguzi mkuu uliokuwa wa huru, haki na wenye kuaminika, nia ambayo amesema bado anayo.

Hotuba ya rais Kabila mbali na kugusia utangamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu, amewapongeza wananchi wa taifa hilo kwa kuendelea kudumisha amani, huku akiapa kuendelea na juhudi za kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana kwenye eneo la mashariki mwa nchi ambalo linakabiliwa na uasi wa makundi ya wapiganaji wenye silaha.

Rais Kabila ameendelea kusisitiza kuwa uchaguzi wa taifa hilo utafanyika kwa misingi ya kidemokrasia na kwamba hakuna suala ambalo litatatiza uchaguzi huo usifanyike kwa muda uliopangwa, kauli inayotoa matumaini ya kufanyika kwa uchaguzi mwaka huu.