SOMALIA

Al Shabab yarusha makombora katika makaazi ya watu mjini Baidoa

Baadhi ya silaha zilitumiwa kutekeleza shambulizi la kigaidi mjini Baidoa
Baadhi ya silaha zilitumiwa kutekeleza shambulizi la kigaidi mjini Baidoa RFI/Stéphanie Braquehais

Watu wawili wameuawa na wengine 18 kujeruhiwa katika mji wa Baidoa, Kusini Magharibi mwa Somalia baada ya kushambuliwa na wanamgambo wa Al Shabab.

Matangazo ya kibiashara

Gavana wa jimbo la Bay Abdirashid Abdullahi, amesema wanamgambo hao walirusha makombora kadhaa kulenga makaazi ya watu katika mji huo.

Ripoti zinasema kuwa makaazi yaliyolengwa ni yale yaliyo karibu na uwanja wa ndege wa Baidoa karibu na kambi ya wanajeshi wa Ethiopia wanaopambana na kundi hilo.

Siku za hivi karibuni, Al Shabab imekuwa ikiwalenga wanajeshi wa AMISOM na kuendeleza mashambulizi dhidi ya viongozi wa serikali mjini Mogadishu.

Kundi la A Shabab liliondolewa katika jiji kuu Mogadishu miaka mitano iliyopita, lakini limeendelea kutekeleza mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara.

Ongezeko la mashambulizi kama haya linajiri wakati huu Somalia ikitarajiwa kuwa na uchaguzi hivi karibuni.

Jeshi la Uganda limetangaza kuwa litarudi nyumbani mwaka ujao baada ya kuwa nchini humo kuanzia mwaka 2007.

Kumekuwa na madai kuwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia hawajalipwa kwa miezi kadhaa sasa.