DRC-SIASA

Katumbi asema atarudi nyumbani hivi karibuni kuongoza maandamano

Mwanasiasa wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi Chapwe ambaye amekuwa nchini Uingereza kupata matibabu amesema atarudi nyumbani kuongoza maandamano ya amani dhidi ya rais Joseph Kabila.

Kiongozi wa upinzani na mgombea urais wa DRC, Moise Katumbi, ambaye amesema rais Kabila hajajibu maswali ya msingi kwenye hotuba yake
Kiongozi wa upinzani na mgombea urais wa DRC, Moise Katumbi, ambaye amesema rais Kabila hajajibu maswali ya msingi kwenye hotuba yake REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Mwezi uliopita, Katumbi alikuhumiwa jela kwa makosa ya kuhusika na uuzaji wa nyumba kwa njia ya ulaghai kwa raia mmoja wa Ugiriki.

Mahakama mjini Lubumbashi ilimhukumu jela miaka 3.

Hata hivyo, Katumbi hajasema ni lini atarajea nyumbani lakini amesema tu kuwa atafika jijini Kinshasa hivi karibuni.

Tayari Katumbi amesema atawania urais dhidi ya Jospeh Kabila ikiwa ataamua kuwania tena.

Thomas Dakin Mwenyekiti wa Mashirika ya kiraia Mashariki katika jimbo la Kivu Kaskazini amesema ni haki ya Katumbi kuandaa maandamano nchini humo ikiwa atarejea.

Katumbi ameendelea kuilaani serikali ya Kinshasa kwa kumlenga kisiasa, ili asiwanie urais.

Serikali ya Kinshasa imeshtumu Katumbi pia kwa kuhatarisha usalama wa nchi hiyo kwa kuwatumia mamluki kutoka Marekani kumlinda.