AFRIKA KUSINI

Oscar Pistorius ahukumiwa kifungo cha miaka 6 jela

Mwanariadha mwenye ulemabu, Oscar Pistorius, akiwa Mahakamani .
Mwanariadha mwenye ulemabu, Oscar Pistorius, akiwa Mahakamani . REUTERS/Phill Magakoe/Pool

Mahakama nchini Afrika Kusini imemhukumu miaka 6 jela mwanariadha mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius kwa kosa la kuumua mpenzi wake Reeeva Stenkamp miaka mitatu iliyopita.

Matangazo ya kibiashara

Jaji Thokozile Masipa amesema baada ya kusikiliza upya rufaa iliwasilishwa na upande wa mashtaka kupinga hukumu ya awali ya miaka mitano jela aliyokuwa amempa Pistorius na baadaye kuachiliwa huru mwaka uliopita, baada ya kuhudumu kwa mwaka mmoja, amefikia uamuzi huo.

Aidha, Jaji Masipa amesema amefikia hukumu hiyo kwa kuzingatia hali ya Pistorius, familia ya Reeva huku akisisitiza kuwa maoni ya raia wa Afrika Kusini hayawezi kuathiri kwa vyovyote vile uamuzi wa Mahakama.

Pamoja na hilo, ameelezea kwa kirefu namna Pistorius alivyoomba msamaha kwa familia na Reeva na alivyoonesha tabia nzuri wakati alipohukumiwa jela hapo awali.

Mawakili wa Familia ya Reeva Stenkamp walikwenda Mahakamani kutaka Pistorius kuhukumiwa upya kwa miaka 15, kwa madai kuwa alikuwa ameua kwa kukusudia baada ya kutoridhika na uamuzi wa awali.

Oscar Pistorius akiwa ametoa miguu yake ya bandia wakati kesi yake ikiendelea siku zilizopita
Oscar Pistorius akiwa ametoa miguu yake ya bandia wakati kesi yake ikiendelea siku zilizopita REUTERS/Siphiwe Sibeko

Pistorius alionekana mwenye huzuni kipindi chote cha usomaji wa hukumu yake kinyume na ilivyokuwa nyakati zilizopita alipoangua kilio Mahakamani.

Utulivu kama huo pia ulishuhudiwa kwenye nyuso za Familia ya Stenkamp ambayo imekuwa ikisema inataka haki kutendeka.

Jaji Masipa, amesisitiza kuwa mazingira ya kesi hii yalizidi malalamishi ya upande wa mashtaka na hukumu yoyote dhidi ya Pistorius haiwezi kurejesha maisha ya Reeva Stenkamp.

Oscar Pistorius amekuwa nje na ndani ya Mahakama na hata kufungwa jela tangu mwaka 2013 na sasa atarejea tena jela kwa muda wa miaka 6 ijayo.

Kwa mujibu wa Katiba nchini Afrika Kusini, ikiwa Pistorius ataonesha tabia nzuri akiwa gerezani anaweza kuachiliwa huru baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu ijayo.

Ripoti zinasema kuwa kiongozi wa mashtaka hana nia ya kukata rufaa kupinga hukumu hii inayoashiria mwisho wa kesi hii.