Sudan Kusini: UNSC yakutana Jumapili 10 Julai
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana katika faragha kwa mashauriano Jumapili saa kumi na nusu saa za New York (sawa na saa 2:30 usiku) Jumapili hii kufuatia mapigano makali mjini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, wanadiplomasia wamesema.
Imechapishwa:
Mapigano ya hivi karibuni kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na wale wa makamu wa rais na kiongozi wa zamani wa waasi Riek Machar yameongezeka Jumapili hii Julai 10.
Hali ni tete katika mji wa Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwa upande wake ametoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini kusitisha mapigano, akisemaa "hayakubaliki."
Maelfu ya wakazi wa mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, wamekua wakikimbia mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi wa zamani, pande zote mbili zinashtumiana kila mmoja kuhusika na machafuko haya mapya.
mapigano hayo, ambayo yamesababisha watu 150 kupoteza maisha katika kipindi cha siku mbili,yanauweka hatarini mkataba wa amani uliyosainiwa mwaka jana katika taifa changa duniani, ambalo liliadhimisha Jumamosi hii Jualai 9 miaka mitano ya uhuru wake. Sudan Kusini inakumbwa tangu mwaka 2013 na vita vikali ambavyo vimegharimu maelfu ya watu na karibu watu milioni tatu wameyahama makazi yao.
Mpaka sasa hakuna idadi ya vifo au hasara yoyote ambayo imetangazwa
Jumapili hii, Umoja wa Mataifa umebaini kwamba, milio ya risasi na milipuko ya mabomu vimesikika katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Helikopta za kivita na vifaru pia vimeonekana kutumiwa katika mapigano hayo.Taarifa hizi zimesababisha maelfu ya watu katika mji mkuu wa nchi hiyo kusalia nyumbani au kuyahama makazi yao, mashahidi wamesema.
"Hali imekua tete katika mji wa Juba," Ubalozi wa Marekani umeonya, ukiwataka Wamarekani walioko nchini Sudani Kusini kusalia nyumbani.
"Mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya serikali na upinzani, hasa karibu na uwanja wa ndege, katika maeneo ya tume ya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini (UNMISS), (katika eneo la Jebel) na katika maeneo mbalimbali mjini Juba ", taarifa ya ubalozi wa Marekani imebaini.