UCHAMBUZI - DRC

Tshisekedi na hatma ya mazungumzo ya DRC

Jopo la wasuluhishi wa mazungumzo ya kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo juma hili, limekutana na Kinara wa upinzani nchini humo Etienne Tshisekedi wa Mulumba, jijini Brussels.

Etienne Tshisekedi akiwa mjini Kinshasa mwaka 2012
Etienne Tshisekedi akiwa mjini Kinshasa mwaka 2012 AFP PHOTO / JUNIOR DIDI KANNAH
Matangazo ya kibiashara

Katika mazungumzo hayo, jopo hilo limeshirikisha wawakilishi wa baadhi ya vyama vya upinzani vinavyounda muungano unaojulikana kwa jina la “Rassemblement” chini ya usimamizi wa Tshisekedi.

Aidha, majadiliano hayo yalilenga utekelezaji wa Azimio Namba 2277 la Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linalotaka mazungumzo ya Congo yafanyike kwa kuheshimu katiba ya nchi hiyo.

Kwa upande wa vyama hivyo vya upinzani, mkazo umewekwa kuhusu uboreshaji wa hali ya kisiasa nchini DRC ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa, usalama wa watakaoshiriki pamoja na kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa.

Sanjari na hayo, pande zote mbili zimekubaliana kuhusu haja ya kuanzisha mazungumzo hayo haraka iwezekanavyo ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai.

Ujumbe wa jopo hilo unajumuisha Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Smail Chergui, Mjumbe Maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa maziwa makuu, Said Djinit, na Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya Afrika wa Umoja wa Ulaya, Koen Vervaeke.

Hatua hii iliofikiwa imepongezwa na serikali ya Marekani ingawa nchi hiyo haina mjumbe katika jopo la wawakilishi kulingana na matakwa ya serikali ya Kinshasa ambaye haikutaka nchi mojamoja kushiriki kama sehemu ya usuluhishi labda kwa kuepuka kuingiliwa kisiasa.

Hata hivyo, lengo kuu kulingana na upande wa serikali ni kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi ujao ili kuepuka vurugu kama zile zilizojitokeza mwaka 2011; ambapo Bw. Tshisekedi amejitangaza kushinda urais na kujiapisha katika makazi yake ya Limete mjini Kinshasa.

Haya yanayoendelea, swali moja linajitokeza ikiwa hatma ya mazungumzo hayo ipo mikononi mwa upinzani na hasa Tshisekedi wa Mulumba ambaye hadi sasa anasubiriwa kuwasilisha orodha ya wajumbe wa upande wa upinzani kwa ajili ya uundwaji wa kamati ya maandalizi ya mazungumzo hayo.
Mwezi uliopita, Tshesekedi na washiriki wake wa upinzani waliweka masharti kwa kushiriki katika mazungumzo hayo ikiwa ni pamoja na kuheshimu matakwa ya katiba ya Congo ikimaanishwa kuandaa uchaguzi unaotakiwa kufanyika tarehe 19 desemba 2016 kwa mujibu wa katiba ya Congo.