SOMALIA

Kiongozi wa Al-Shabab aituhumu Uturuki kuhusika na uchochezi nchini mwake

Wapiganaji wa Al-Shabab na wale wa Hizbul Islam, mjini Mogadishu, Julai 21, 2009.
Wapiganaji wa Al-Shabab na wale wa Hizbul Islam, mjini Mogadishu, Julai 21, 2009. (Photo : AFP)

Kiongozi wa kundi la Al-Shabab la nchini Somalia, Ahmed Diriye, ameitaja nchi ya Uturuki kama "adui wa taifa lake" na kuvituhumu vikosi vya kimataifa vya kulinda amani, kuwa vinalinyonya taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Katika ujumbe wake wa kwanza kuutoa tangu achukue uongozi wa kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa Al-Qaeda, baada ya kifo cha kamanda wake aliyeuawa kwenye shambulio la majeshi ya Marekani mwaka 2014, Diriye anasema uwepo wa Uturuki kwenye taifa lao ni kutaka "kupora rasilimali za Somalia kuliko kusaidia".

Kundi la Al-Shabab linapigana kutaka kuiondoa madarakani Serikali inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa, na mara kadhaa limekiri kuhusika na mashambulizi ya kujitoa muhanga mjini Mogadishu na maeneo mengine ya nchi.

Katika ujumbe wake uliorekodiwa kwa dakika 44 na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kutangazwa na Redio ya kundi hilo, Diriye pia amevituhumu vikosi vya kulinda amani nchini humo kwa kuendelea kufanya vitendo vikubwa vya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wa Somalia.

"Somalia imevamiwa na watetezi wa Ukristo, wanaojiita Jumuiya ya Kimataifa ambayo inawadanganya wananchi wa Somalia kuikubali Ethiopia na AMISOM, wakiwa na lengo la kuitawala wa Somalia na kupora Mali," alisema Diriye.

"Utawala wa Uturuki ni adui wa taifa letu, leo hii uchumi wa Somalia umevurugika kutokana na uvamizi wao...Uturuki imevamia nchi yetu kiuchumi...wamechukua uongozi wa uchumi wetu na kile ambacho wanakitaka ni kuiacha Somalia iwe masikini."

Hivi karibuni nchi ya Uturuki imeongeza mchango wake kwa nchi ya Somalia, ambapo inatoa mchango mkubwa kusaidia kuijenga nchi ya Somalia na kusaidia programu za misaada ya kibinadamu, wafanya biashara wa Uturuki wanamiliki biashara kubwa kwenye bandari kuu na uwanja mkuu wa ndege wa Somalia.