UCHAMBUZI - DRC

Rais Joseph Kabila si kinara pekee wa siasa za Congo

Joseph Kabila akiwa mjini Washington mwaka 2014.
Joseph Kabila akiwa mjini Washington mwaka 2014. AFP PHOTO/JIM WATSON

Swali la msingi linaloulizwa na wadau wa siasa za DRC ni kuhusu nafasi ya Rais Kabila katika siasa za nchi hiyo wakati huu DRC inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya wito kutoka Jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Azimio namba 2277 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka uchaguzi nchini DRC ufanyike kulingana na Katiba, uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika Novemba 27, kiuhalisia uwezekano wa kuwa uchaguzi utafanyika kwa wakati huenda ikawa ni ndoto ya mchana ikizingatiwa muda unavyoendelea kuyoyoma.

Kwa miezi kadhaa sasa, upinzani nchini humo umeilalamikia Serikali inayoongozwa na Rais Joseph Kabila kutaka kujiongezea muda wa kuendelea kubaki madarakani kinyume na katiba ya Congo, jambo ambalo halijawahi kuzungumziwa na Rais mwenyewe.

Barack Obama, Rais wa Marekani
Barack Obama, Rais wa Marekani REUTERS/Jonathan Ernst

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo, CENI, uchaguzi wa rais na chaguzi nyingine, vinaweza kufanyika katika miezi 14 au 16 ijayo, muda ambao tume itautumia kupata fedha za maandalizi na kufanya mapitio ya daftari la wapiga kura kwa lengo la kuwajumuisha ambao wamefikiwa umri wa miaka kumi na nane.

Kutokana na utata uliopo, Rais Kabila ametoa wito kwa wakosoaji wake kukaa kwenye meza ya mazungumzo, lakini upinzani ambao upo mbioni kuimarisha umoja wake, unataka mazungumzo hayo ya kisiasa yafanyike kwa mujibu wa Azimio namba 2277 la Baraza la Usalama, kuheshimu mipaka ya kikatiba ya kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge wa kitaifa pamoja na kuachiwa huru kwa wafungwa wa kisiasa.

Aidha, Upinzani unasema ikiwa malengo yanataka kufikiwa, basi masuala muhimu ni lazima yashughulikiwe, ambapo unapinga marekebisho yoyote ya kikatiba na kutaka hali ya haki za binadamu iboreshwe kama moja ya masharti kwa kushiriki kwenye mazungumzo hayo.

Kwa kuzingatia hayo yote, Je, Rais Joseph Kabila bado ni kinara wa siasa za Congo?

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa za ukanda wa Maziwa Makuu wameanza kuamini kuwa usukani wa siasa za nchi hiyo na hatma yake, pamoja na kwamba vinategemea utashi wa kisiasa wa raia wa Congo wenyewe, bado mkono wa wadau wa nje ya nchi hiyo utaendelea kuelekeza mwelekeo wa mambo.

Mbali na azimio la Umoja wa Mataifa, Serikali ya Marekani, mwezi uliopita, imeanza kutoa adhabu za kufungia mali za viongozi wanaodaiwa kushiriki katika kuminya demokrasia na uhuru wa watu kwa kuanzia na Jenerali wa Polisi Kanyama maarufu kwa jina la “Esprit de Mort” au Roho ya Kifo.

Sanjari na hayo, Serikali ya Rais Kabila, bado inaendelea kutegemea misaada kutoka nje, hususani nchi za magharibi kufadhili Tume ya uchaguzi kulingana na ahadi zilizotolewa na baadhi ya wadau na nchi wahisani.

Meja-Jenerali  MUSHALE wa Monusco akiwa mjini Beni, DRC.
Meja-Jenerali MUSHALE wa Monusco akiwa mjini Beni, DRC. MONUSCO/Force

Rais Joseph Kabila, ambaye Serikali yake ililazimika mwezi uliopita kupitia upya Bajeti yake ya mwaka 2015-2016 kwa lengo la kupunguza matumizi, inakumbwa na ukata kufuatia kuporomoka kwa bei na thamani ya madini kwenye soko la nje la madini yanayotegemewa na serikali hiyo.

Kwa hali ilivyo, Rais Kabila, atalazimika kukubali msaada wowote kutoka kwa wahisani ikiwa ni pamoja na nchi za magharibi zinazokosolewa na serikali yake kuingilia masuala ya ndani ya Congo pia na msaada wa hali na mali kutoka kwa vikosi vya kulinda amani nchini humo MONUSCO ambavyo vimeelezea utayari wake kusaidia uchaguzi kufanyika kwa ufanisi.

Kwa minajili hiyo, Rais Joseph Kabila, si kinara pekee wa siasa za Congo hasa ikizingatiwa hali inavyoendelea kuonekana nchini humo, kwamba haitegemei uwezo wala nguvu za upande mmoja lakini jumuisho la utashi wa wadau wote wa ndani na nje ya nchi hiyo ya pili barani Afrika kwa ukubwa.