SUDAN

UN yazindua kampeni ya kusaka fedha kusaidia maelfu ya raia Darfur

Mwanamke mmoja akiwa ameketi nje ya nyumba yake iliyoteketea kwa moto kwenye jimbo la Darfur Kusini.
Mwanamke mmoja akiwa ameketi nje ya nyumba yake iliyoteketea kwa moto kwenye jimbo la Darfur Kusini. REUTERS/Albert Gonzalez Farran/ys

Umoja wa Mataifa umezindua rasmi kampeni ya kidunia ya kukusanya kiasi cha dola za Marekani, milioni 952, kwa lengo la kuisaidia nchi ya Sudan kukabiliana na janga la kibinadamu mwaka 2016, wengi wa waathirika wakitoka kwenye jimbo la Darfur. 

Matangazo ya kibiashara

Mpango huu ambao ulicheleweshwa ili kuzungumzia mahitaji ya kibinadamu kwa watu zaidi ya milioni 4 na laki 6, wakiwemo maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini ambao wamekimbilia Sudan, wakikimbia machafuko na uhaba wa chakula kwenye nchi yao.

"Wanawake, wanaume, wakimbizi na wakimbizi wa ndani, wanatutaka sisi kuongeza juhudi kutoa msaada kwao," amesema Naeema Al-Gasseer, mratibu wa misaada ya kibinadamu kwa nchi ya Sudan.

Al-Gasseer, ameongeza kuwa fedha zitakazopatikana, zitatumiwa kufikia malengo ya mahitaji ya kinadamu kwa watu walionaswa kwenye machafuko jimboni Darfur.

Machafuko kwenye jimbo la Darfur yalianza mwaka 2003 wakati jamii ya makabila madogo kwenye eneo hilo, walipoanza kushika silaha kumpinga Rais Omar al-Bashir, wanayemtuhumu kupendelea waarabu.

Kufuatia uasi huo, Rais Bashir na Serikali yake walianzisha vita kuwakabili watu waliokuwa wanaipinga Serikali yake, ambapo zaidi ya watu laki 3 waliuawa kutokana na vita hivyo, huku umoja wa Mataifa ukisema kuwa zaidi ya watu wengine milioni 2 na laki 5 wakikimbia nyumba zao.