MAJI

Euro Bilioni 1.6 kusaidia upatikanaji wa maji safi barani Afrika

Mama akiteka  maji chafu kwa matumizi ya nyumbani
Mama akiteka maji chafu kwa matumizi ya nyumbani Wordmag.com

Viongozi wa bara Afrika wametakiwa kuyapa maji safi kipaumbele, ikiwa wanataka kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kufikia mwaka 2030.

Matangazo ya kibiashara

Wito huu umetolewa katika kongamano la Sita la maji barani Afrika uliomalizika siku ya Ijumaa jijini Dar es salaam nchini Tanzania.

Akifunga mkutano huo, Makamu wa rais wa Tanzania Bi. Samia Suluhu amesema bila ya kuwepo kwa maji safi ya matumizi, umasikini na usawa hauwezi kufikiwa barani Afrika.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Mawaziri wa maji kutoka mataifa yote barani Afrika ambao walikutana katika mkutano wao wa 10 kujadili ni vipi bara la Afrika linaweza kupata maji safi ya matumizi.

Wito kama huu pia umetolewa na Bi. Rhoda Peace Tumusiime, Katibu anayehusika na tume inayoshughulikia maswala ya uchumi vijijini na kilimo katika Umoja wa Afrika (AMCO).

Aidha, amewahimiza viongozi wa Afrika kutunga sera na sheria zitakazosaidia upatikanaji wa maji safi ikiwa ni pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia na kutambua haki za wanawake.

Rais mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki(Kushoto) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa (Kulia) wakati wa kongamano la maji jijini Dar es salaam
Rais mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki(Kushoto) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa (Kulia) wakati wa kongamano la maji jijini Dar es salaam 4.bp.blogspot.com

Kongamano hilo la wiki moja limebainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa waafrika wengi kupata maji safi ya kunywa, na kufikia hilo zaidi ya Euro Milioni 44 zinahitajika ili kufanikisha malengo hayo.

Akizungumza mapema wiki hii wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Waziri wa Maji wa Nigeria Mhandisi Suleiman Adamu, ambaye alikuwa anamaliza muda wake kama rais Waziri wa Maji barani Afrika, alitangaza kuwa, kituo cha maji barani Afrika kimetoa Euro Bilioni 1.6 kufanikisha mradi wa upatikanaji wa maji safi barani Afrika, mradi ambao unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya watu Milioni 3 nukta 2.

Waziri wa Maji nchini Tanzania Gerson Lwenge, anachukua urais wa baraza la Mawaziri wa maji barani Afrika (AMCOW) kuongoza ajenda ya upatikanaji wa maji safi ya kunywa barani Afrika.