DRC-SIASA

Wanaharakati wa LUCHA wakataa msamaha wa rais Kabila

Wanaharakati sita wa kisiasa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo LUCHA, waliopewa msamaha na serikali wamekataa kuondoka Gerezani. 

Wanaharakati wa Lucha wakiwa Mahakamani katika siku zilizopita mjini Goma
Wanaharakati wa Lucha wakiwa Mahakamani katika siku zilizopita mjini Goma ibtimes.co.uk
Matangazo ya kibiashara

Vijana hao wamekuwa wakizuiliwa tangu mwezi Machi mwaka huu mjini Goma, Mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza harakati za kumtaka rais Joseph Kabila kujiuzulu na kutowania urais kwa muhula wa tatu.

Trésor Akilimali mmoja wa vijana hao amesema hawataki msamaha wa rais Kabila na watasalia Gerezani hadi pale wafungwa wengine wa kisiasa watakapoachiliwa huru na muda wao kukamilika.

"Ndugu zetu hapa Goma wamesema watabaki kifungoni hadi wenzetu wote ambao wamefungwa wataachiliwa huru,” alisema.

Stephano Mashukano mmoja wa viongozi wa chama cha upinzani cha UNC katika jimbo la Kivu Kaskazini ameunga mkono hatua hiyo ya wanaharakati hao kwa kusema hakuna haja ya msamaha huo wiki mbili tu kabla ya muda wao wa kufungwa Gerezani kumalizika.

“Hatuelewi inakuwaje, wanaachiliwa huru ikiwa imebaki wiki mbii au tatu waondoke, waendelee kusalia gerezani hadi muda wao utakapomalizika,” alisema Mashukano.

Hata hivyo, serikali kupitia Waziri wa Sheria na Haki Alexis Mwamba amesema ni lazima wanaharakati hao waondoke Gerezani hata kama nguvu itatumika.

“Ni lazima waondoke kwa sababu hakuna haja ya kuendelea kuwazuai kwa sababu msamaha wa rais ni hatua ambayo haiwezi kupingwa na yeyote,” alisema Mwamba.

Haya yanajiri wakati huu nchi hiyo ikijiandaa kuwa na mazungumzo ya kitaifa mwishoni mwa mwezi huu, mazungumzo ambayo muungano wa upinzani umesema hautashiriki.

Hii ni ripoti ya Mwandishi wetu wa Mashariki mwa DRC Chube Ngorombi.