DRC

Koffi Olomide akamatwa jijini Kinshasa

Mwanamuziki maarufu  kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Koffi Olomide, amekamatwa jijini Kinshasa kwa kosa la kumpiga teke mnenguaji wake wa kike jijini Nairobi nchini Kenya mwishoni mwa juma lililopita.

Koffi Olomide akikamatwa jijini Kinshasa
Koffi Olomide akikamatwa jijini Kinshasa The Star
Matangazo ya kibiashara

Masaibu ya Olomide yameendelea kushuhudiwa kwa juma la pili baada ya kukamatwa na kufukuzwa nchini Kenya kutokana na tukio hilo, na tamasha lake kusitishwa.

Waandalizi wa tamasha lingine nchini Zambia hapo jana walitangaza pia kusitisha tamasha la mwanamuziki huyu baada ya tukio hilo.

Polisi nchini DRC wanasema mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 60 anashikiliwa kwa mahojiano zaidi kutokana na tukio la Nairobi.

Jumapili iliyopita, Olomide alihojiwa na Televisheni moja nchini humo akiomba msamaha kwa kitendo alichofanya.

Hii sio mara ya kwanza kwa mwanamuziki huyu kujipata katika hali hii.