SOMALIA

Watu 13 wauawa mjini Mogadishu kutokana na mashambulizi ya Al Shabab

Shambulizi la kigaidi  mjini Mogadishu
Shambulizi la kigaidi mjini Mogadishu Reuters/Feisal Omar

Mashambulizi mawili ya bomu yamesababisha vifo vya watu 13  katika uwanja wa ndege mjini Mogadishu nchini Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema kuwa mlipuko mmoja ulisikika katika uwanja huo wa ndege karibu na jengo la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

“Watu 13 wameuawa katika mashambulizi haya mawili, na gari moja lilipuka nje ya jengo la Umoja wa Mataifa,” amesema Biashar Abdi Gedi afisa wa polisi.

Aidha, ameongeza kuwa wanajeshi wa AMISOM walijitahidi na kupambana na magaidi wa Al Shabab ambao baadaye walitoweka.

Mashambulizi kama haya nchini Somalia yamekuwa yakitekelezwa mara kwa mara na kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo kwa muda mrefu limesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Uwanja huo wa ndege unakaribiana sana na makao makuu ya kambi Umoja wa Afrika ya wanajeshi wa kulinda amani AMISOM.

Kundi la Al Shabab linasema linataka kuipindua serikali inayosema ni ya nchi za Magharibi lakini pia inataka kuondoka kwa vikosi vya AMISOM vinavyokadiriwa kuwa 22,000.