DRC-SIASA

Etienne Tshisekedi arejea nyumbani na kupokelewa na maelfu ya wafuasi wake

Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Etienne Tshisekedi ambaye amekuwa akiishi nchini Ubelgiji kwa miaka miwili sasa amerejea nyumbani.

Kiongozi wa upinzani  Etienne Tshisekedi akiwasili jijini Kinshasa tarehe 27 Julai  2016.
Kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi akiwasili jijini Kinshasa tarehe 27 Julai 2016. RFI/Sonia Rolley
Matangazo ya kibiashara

Maelfu ya wafuasi wake kuanzia asubuhi wakiwa wamebeba mabango ya kumkaribisha na kuvalia fulana ziliandikwa jina lake walifurika katika uwanja wa ndege jijini Kinshasa kumsubiri kiongozi wao.

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 83 amerejea nyumbani wakati huu kukiwa na mkanganyiko ikiwa kutakuwa na uchaguzi nchini humo mwaka huu.

Aidha, anawasili baada ya siku kadhaa kutangaza kuwa muungano wa upinzani hautashiriki katika mazungumzo ya kitaifa kuhusu hali ya kisiasa, mazungumzo  yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Tshisekedi amekuwa katika ulingo wa kisiasa nchini DRC kwa kipindi kirefu tangu miaka ya 80 alipokuwa anampinga kiongozi wa wakati huo Mobutu Sese seko.

Mwaka 2011 aliwania urais, uchaguzi ambao alidai alishinda lakini kura zikaibiwa na kumpa ushindi rais wa sasa Joseph Kabila.