DRC-SIASA

Jaji nchini DRC asema alishinikizwa kumhukumu jela Katumbi

Kiongozi wa upinzani na mgombea urais wa DRC, Moise Katumbi, ambaye amesema rais Kabila hajajibu maswali ya msingi kwenye hotuba yake
Kiongozi wa upinzani na mgombea urais wa DRC, Moise Katumbi, ambaye amesema rais Kabila hajajibu maswali ya msingi kwenye hotuba yake REUTERS

Mmoja wa Majaji mjini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye alikuwa miongoni mwa Majaji watatu waliotoa hukumu ya kumfunga jela miaka mitatu Gavana wa zamani wa jimbo la Katanga Moise Katumbi Chapwe, amesema alishinikizwa kutoa hukumu hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Jaji huyo kiongozi Chantale Ramazani Wazuri ambaye ripoti zinasema tayari ameondoka nchini humo, amewaandika barua wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika nchini humo kulalamikia shinikizo alizopata kutoka kwa wenzake.

Mbali na hukumu hiyo dhidi ya mwanasiasa huyo wa upinzani aliyekuwa nje ya nchi wakati ilipotolewa, Jaji huyo ameongeza kuwa hukumu hiyo inamtaka Katumbi kukamatwa ikiwa atarejea nchini humo.

Katika barua hiyo, Jaji huyo amesema hukumu hiyo ilikuwa ya kisiasa yenye lengo la kuhakikisha kuwa hawanii urais nchini humo mwaka huu.

Katumbi amekuwa akisema kuwa kesi dhidi yake ni ya kisiasa baada ya kutangaza kuwa atawania urais nchini humo.

Mwansiasa huyo wa upinzani ametangaza kuwa atarejea nyumbani kuendeleza siasa zake lakini serikali imesema kuwa itamkamata na kumshtaki kwa kosa la kuhatarisha usalama wa taifa.