ZIMBABWE

Msemaji wa wapiganiaji uhuru nchini Zimbabwe akamatwa na polisi

Msemaji wa wapiganiaji wa uhuru nchini Zimbabwe Douglas Mahiya
Msemaji wa wapiganiaji wa uhuru nchini Zimbabwe Douglas Mahiya nehandaradio

Polisi nchini Zimbabwe wamemkamata Douglas Mahiya, msemaji wa umoja wa wapiganiaji wa zamani wa uhuru wa nchini humo  baada ya kumtuhumu rais Robert Mugabe kuwa Dikteta.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji hao wa zamani ambao walishirikiana na rais Mugabe katika vita hivyo vya uhuru miaka ya 70, wiki iliyopita walijitokeza na kumshutumu kiongozi huyo kuwa na tabia za kidikteta katika uongozi wake lakini pia kuwasahau.

Kukamatwa kwa msemaji huyo kumethibitishwa na Mawakili wa kutetea haki za binadamu nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa Mahiya alikamatwa jijini Harare jana jioni na polisi wanamshtumu kwa kosa la kukiuka katiba na kuikosea heshima Ofisi ya rais nchini humo.

Kukamatwa kwake kunakuja siku moja baada ya rais Mugabe kusema kuwa wale wote wanaohusika na madai ya  wapiganaji hao wa zamani watachukuliwa hatua kali.

Polisi jijini Harare imekataa kusema ni wapi wanakomshikilia msemaji huyo.

Wazee hao wamekuwa wakimshutumu rais Mugabe mwenye umri wa miaka 92 na ambaye ameongoza nchi hiyo tangu mwaka 1980 kwa kukataa kutambua juhudi zao na kuwafidia.