UN-BURUNDI

Warundi waandamana kupinga azimio la UN kupeleka askari

Waandamanaji jijini Bujumbura wakielekea katika ofisi za ubalozi wa Ufaransa kupinga uamuzi wa UN
Waandamanaji jijini Bujumbura wakielekea katika ofisi za ubalozi wa Ufaransa kupinga uamuzi wa UN STR / AFP

Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza mitaani jijini Bujumbura jumamosi kupinga uamuzi wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kutuma kikosi cha askari maalum wa umoja wa mataifa katika taifa hilo linalokabiliwa na ghasia.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano mjini Bujumbura yaliandaliwa na utawala kulingana na chanzo kimoja cha kidiplomasia ambapo kimeeleza kuwa yalipitika kwa amani lakini yalibeba ujumbe wa serikali dhidi ya pendekezo la kikosi cha askari 228 wa UN.

Mamlaka mjini humo zinasema idadi ya waandamanaji ilifikia elfu kumi.

Waandamanaji waliffika katika ofisi za ubalozi wa Ufaransa wakiwa na hasira juu ya Ufaransa ambayo ilipendekeza maazimio hayo ya kupeleka kikosi tata cha UN.

Muandamanaji mmoja alibeba bango lililoandikwa Ufaransa ni muhitaji wa walinda amani wa UN akikariri shambulizi la lori mjini Nice nchini Ufaransa hivi karibuni lililoua zaidi ya watu 80 mapema mwezi huu.

Balozi wa Ufaransa Gerrit van Rossum, ambaye alitoka kuwahutubia alisema tatizo ni kutokuelewa kwa kiasi kikubwa kuhusu wajibu wa ufaransa katika baraza la usalama la umoja wa mataifa.Alisema hakukuwa na tatizo katika maandamano hayo.

Meya wa Bujumbura Freddy Mbonimpa ameiambia AFP kuwa hawaelewi msisitizo wa Ufaransa katika jambo hilo hususan wakati huu ambapo Umoja wa Afrika umoja wa mataifa na viongozi wa mataifa wamekwisha zuru Burundi na kukuta maisha yamerejea katika hali ya kawaida.