AFRIKA KUSINI

ANC yapata matokeo mabaya kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliyeshika kofia akiwapungia mkono wafuasi wa chama chake cha ANC hivi karibuni
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma aliyeshika kofia akiwapungia mkono wafuasi wa chama chake cha ANC hivi karibuni REUTERS/Siphiwe Sibeko

Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Serikali za mitaa nchini Afrika Kusini, yametoa pigo kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), wakati huu matokeo ya awali yakionesha kuanguka vibaya kwa chama hicho kilichomaliza ubaguzi wa rangi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huu karibu asilimia 80 ya kura zote zikiwa zimehesabiwa, chama cha ANC kinaongoza kwa ujumla nchi nzima, lakini kimerekodi matokeo mabaya zaidi kuwahi kutokea toka kumalizika kwa utawala wa kibaguzi miaka 22 iliyopita.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance DA kilikuwa kinaongoza kwenye mji wa Cape Town pamoja na Port Elizabeth, huku mji wa Pretoria na Johannesburg chama chicho kikichuana kwa karibu na chama tawala ANC.

Chama cha ANC kimeshinda kwa asilimia 60 katika kila chaguzi zilizofanyika nchini humo toka mwaka 1994, huku hapo jana matokeo ya awali yakionesha kikipata asilimia 54, kikifuatiwa na chama cha DA chenye asilimia 27 huku chama cha Julius Malema, EFF, kikipata asilimia 7.

Mmoja wa wanachama wa ANC akipiga kura kwenye uchaguzu ulifanyika, Agosti 3, 2016 nchini Afrika Kusini
Mmoja wa wanachama wa ANC akipiga kura kwenye uchaguzu ulifanyika, Agosti 3, 2016 nchini Afrika Kusini REUTERS/James Oatway

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa chama tawala kinapoteza nguvu, lakini kinaweza kuvishawishi vyama vingine vidogo kuunda muungano, huku wakieleza kuwa siasa za nchi hiyo zinabadilika na huenda zikabadilika zaidi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2019.

Uchaguzi wa Jumatano ya wiki hii, ulikuwa pia kama hukumu kwa rais Jacob Zuma, ambaye amekuwa akikabiliwa na mfululizo wa kashfa toka ameingia madarakani mwaka 2009.