DRC

Rais Kabila ataka kuundwa upya kwa tabaka la kisiasa

Rais wa DRC, Joseph Kabila mwenye kaunda suti (Kushoto), akiwa na Gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini (kulia) Julien Paluku, wakati alipotembelea mji wa Beni hivi karibuni
Rais wa DRC, Joseph Kabila mwenye kaunda suti (Kushoto), akiwa na Gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini (kulia) Julien Paluku, wakati alipotembelea mji wa Beni hivi karibuni RFI

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joesph Kabila ambae anafanya ziara mashariki mwa nchi hiyo, ametoa wito wa kuundwa upya kwa tabaka la kisiasa.

Matangazo ya kibiashara

Rais Kabila, amesema haya wakati akiwa katika mji wa Beni ambapo amekutana na wanaharakati wa mashirika ya kiraia pamoja na viongozi wa kidini.

Mazungumzo yake na wajumbe hao yalihusu suala la Usalama mdogo katika eneo hilo ambao umekuwa ukitatizika mara kwa mara.

Mchungaji Gilbert Kambale Kamate ambae ni mwenyekiti wa mungano wa mashirika ya kiraia mjini Beni amemtaka rais Kabila kutekeleza ahadi zake.

Wanaharakati hao wanasema kuwa kwa sehemu kubwa hali ya usalama imeendelea kuzorota kwenye eneo hilo, kutokana na ukweli kuwa vikosi vya Serikali vimekuwa vikizembea kuimarisha usalama, hali inayoruhusu makundi ya waasi kutekeleza uasi.

Rais Kabila, amesema kuwa Serikali yake inafanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya usalama inarejea kwenye eneo la mashariki, na kuongeza kuwa hivi karibuni kitatumwa kikosi cha wanajeshi maalumu waliopewa mafunzo kukabiliana na waasi.

Kiongozi huyo, amekiri kuwa hali ya usalama kwenye eneo la mashariki ni miongoni mwa mambo yanayomnyima usingizi, na kwamba atahakikisha kuwa usalama unaimarishwa kwenye maeneo yote ya nchi.

Amewataka wananchi pamoja, viongozi wa dini na wakuu wa mashirika ya kiraia, kushirikiana na Serikali yake katika kuhakikisha wanayamaliza makundi ya waasi kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kutambuliwa na kuharibiwa kwa makambi yao.

Rais Kabila amesema haya siku chache tu zikiwa zimepita, toka akutane na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambapo pamoja na mambo mengine walijadili hali ya usalama kwenye eneo la mashariki mwa DRC, ambako kundi la waasi wa Uganda wa ADF Nalu limekuwa likitekeleza mauaji ya kiholela dhidi ya raia.

Licha ya operesheni za pamoja za vikosi vya Serikali FARDC na vile vya umoja wa Mataifa, MONUSCO, bado makundi ya waasi yameweza kujipenyeza na kujificha kwenye misitu mikubwa ya mashariki mwa nchi hiyo na kutekeleza uasi.

Rais Josephu Kabila anakaribia kumaliza muhula wake wa kukaa madarakani, huku wakosoaji wake wakidai kuwa suala la usalama mashariki mwa nchi hiyo limemshinda kiasi ataondoka madarakani bila ya suluhu yenyewe kupatikana.

Rais Kabila pia alitumia mwanya huo kuwahakikishia wananchi wa Beni na maeneo mengine kuwa uchaguzi utafanyika kwa muda uliopangwa na kwamba maandalizi yatakapokamilika wananchi watajulishwa tarehe rasmi ya kufanyika kwa uchaguzi wenyewe.