ZAMBIA

Wananchi wa Zambia wanapiga kura kwenye uchaguzi wa kihistoria

Mmoja wa raia wa Zambia akipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge, madiwani na magavana nchini Zambia, 2016
Mmoja wa raia wa Zambia akipiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge, madiwani na magavana nchini Zambia, 2016 DR

Wananchi wa Zambia wanapiga kura Alhamisi hii, katika uchaguzi ambao ulikumbwa na vurugu za hapa na pale kati ya wafuasi wa vyama viwili vikubwa vinavyopewa nafasi, chama tawala cha PF na wale wa upinzani wa UPND. 

Matangazo ya kibiashara

Ikiwa ni miezi 18 tu imepita toka Rais Edgar Lungu ashinde kwenye uchaguzi ambao ushindi wake ulikuwa finyu, yeye pamoja na mpinzani wake wa karibu Hakainde Hichilema, wanakutana tena kwenye kinyang'anyiro kingine, ambapo wagombea 9 wanashiriki.

Kura elfu 27 pakee ndizo zilizowatenganisha wagombea hawa kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka 2015.

Kituo cha kutangazia matokeo ya uchaguzi nchini Zambia, 2016
Kituo cha kutangazia matokeo ya uchaguzi nchini Zambia, 2016 DR

Watu watatu wameripotiwa kuuawa wakati wa kampeni, huku vurugu za mara kwa mara zikishuhudiwa kati ya wafuasi wa chama tawala cha PF cha Rais Edgar Lungu na wale wa upinzani wa chama cha UPND wa Hakainde Hichilema.

Kuelekea uchaguzi wa Alhamisi, Agosti 11, tume ya taifa ya uchaguzi nchini Zambia, ilitoa taarifa kwa uma, ikikosoa vurugu ambazo zimeshuhudiwa, huku ikisema kuwa zimetia doa hali ya amani na utulivu pamoja na demokrasia iliyokuwa imeshamiri kwenye taifa hilo.

Mwezi uliopita, kampeni zililazimika kusitishwa kwa muda wa siku kumi katika jiji la Lusaka, baada ya kutokea makabiliano makali kati ya wafuasi wa chama tawala cha PF na wale wa UPND.

DR
DR The Post Zambia

Hata hivyo vurugu bado zimeshuhudiwa hata wakati wa zoezi lenyewe la kupiga kura kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, huku siku ya Jumatano, wafuasi wa upinzani wakijikuta pabaya wakati mgombwa wao alipokuwa akihitimisha kampeni.

Mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni, yanamaanisha kuwa mshindi wa kinyang'anyiro hiki ni lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, vinginevyo watalazimika kwenda kwenye duru ya pili ya uchaguzi.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa uchaguzi huu ni wa kwanza kuwa na shinikizo kubwa za wafuasi wa pande mbili, ambapo mchuano unatarajiwa kuwa mkali huku wengi wakishindwa kubashiri hali ya mambo itakavyokuwa licha ya upinzani kupewa nafasi.