SOMALIA

Gari lililokuwa limebeba vilipuzi lalipuka mjini Mogadishu na kumuua mtu mmoja

Mojawapo ya athari ya mashambulizi ya kigaidi nchini Somalia
Mojawapo ya athari ya mashambulizi ya kigaidi nchini Somalia Reuters/Omar Faruk

Gari dogo lililokuwa limebeba vilipuzi limelipuka mjini Mogadishu nchini Somalia na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wanne kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Ibrahim Mohammed, afisa wa polisi mjini humo amethibitisha kutokea kwa mlipuko huo na kueleza kuwa polisi walikuwa wanalifukuza gari hilo wakati mlipuko huo ulipotokea.

Aidha, ameongeza kuwa maafisa wa usalama walifanikiwa kuharibu mpango wanaosema ulilenga kuwashambulia raia mjini humo.

Abdulahi Osman aliyeshuhudia mkasa huo amesema kulikuwa na ufwatulianaji wa risasi kabla ya dereva wa gari hilo dogo kutoroka na kuliacha gari hilo kulipuka.

Kundi la kigaidi la Al Shabab halijajitokeza kudai kutekeleza shambulizi hili lakini linafahamika kuendeleza mashambulizi kama haya na kusababisha mauaji ya raia wa nchi hiyo.

Lengo la Al Shabab ni kuiangusha serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ili kuongoza nchi hiyo kufuata utaratibu wa sharia.

Wanajeshi wa AMISOM kutoka mataifa mbalimbali ya bara Afrika kuanzia mwaka 2007 wamekuwa wakipambana na magaidi hao.