Pata taarifa kuu
SUDAN KUSINI

UN yaanzisha uchunguzi kwa askari wake wa UNMISS, Machar apatiwa matibabu Khartoum

Walinda amani wa umoja wa Mataifa walioko mjini Juba, UNMISS, wakionekana kwenye picha wakati fulani walipotekeleza zoezi la kunyang'anya silaha mjni Juba, sasa wanakosolewa kushindwa kuwalinda raia
Walinda amani wa umoja wa Mataifa walioko mjini Juba, UNMISS, wakionekana kwenye picha wakati fulani walipotekeleza zoezi la kunyang'anya silaha mjni Juba, sasa wanakosolewa kushindwa kuwalinda raia UN Photo/Eric Kanalstein
Ujumbe kutoka: Emmanuel Richard Makundi
Dakika 2

Jenerali mstaafu kwenye jeshi la Uholanzi ataongoza jopo huru la uchunguzi kubaini ikiwa walinda amani wa umoja wa Mataifa walishindwa kuwalinda raia wakati wa mapigano makali yaliyozuka kusini mwa mji mkuu wa Sudan Kusini, mwezi uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Meja jenerali Patrick Cammaert atawasilisha ripoti ya uchunguzi huo ndani ya mwezi mmoja kwa katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambapo matokeo yake yatawekwa wazi kwa uma, amesema msemaji wa umoja wa Mataifa.

Vikosi vya umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini vimejikuta kwenye shinikizo kubwa vikikosolewa kwa madai kuwa vilishindwa kuwalinda raia wakiwemo wanawake na wasichana ambao walibakwa jirani kabisa na kambi ya vikosi hivyo kwenye mapigano ya mwezi Julai mjini Juba.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa umerekodi visa zaidi ya 200 vya ubakaji vilivyotekelezwa mwezi Julai peke yake na wanajeshi wa Serikali ambao ni watiifu kwa Serikali ya Rais Salva Kiir.

Mwezi uliopita, katibu mkuu Ban Ki Moon alitangaza kuwa ataanzisha uchunguzi huru kuhusu taarifa za walinda amani hao kushindwa kufika kwa wakati kuwasaidia raia waliohitaji msaada wakati wa mapigano na pia kuchunguza mashambulizi tofauti kwenye hoteli moja mjini Juba.

Wanajeshi wa Sudan Kusini wanatuhumiwa kuwabaka wanawake, kuwadhalilisha wafanyakazi wa umoja wa Mataifa na kumoiga risasi mwandishi wa habari kwenye shambulio la Julai 11 kwenye hoteli ya Terrain mjini Juba, ambapo walinda amani hao wanadaiwa kushindwa kufika kutoa msaada.

Uchunguzi huo utabaini ikiwa walinda amani wa umoja wa Mataifa walioko nchini Sudan Kusini wanaofahamika kama UNMISS, walidhibiti hali kimaadili na kuwalinda raia kwa muda muafaka, alisema msemaji wa umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Sudan Kusini na kiongozi wa waasi Riek Machar, amewasili mjini Khartoum, Sudan, kwaajili ya matibabu, imesema taarifa ya Serikali ya Sudan, baada ya kiongozi huyo kukimbilia nchini DRC.

Nafasi ya Machar, ilichukuliwa na Taban Deng Gai baada ya mamia ya watu kupoteza maisha kwenye mapigano ya mwezi Julai yaliyosababisha Machar kukimbia Juba.

Msemaji wa Serikali ya Khartoum amesema kuwa, Machar amewasili nchini humo kama raia wengine wanaohitaji msaada wa kibinadamu na kwamba atapatiwa matibabu.

Hata hivyo Serikali ya Khartoum haikuweka wazi ni lini kiongozi huyo aliwasili nchini humo, lakini ikasema kuwa alikuwa akihitaji msaada wa haraka wa kimatibabu.

Utawala wa Khartoum unasema kuwa, hali yake imeimarika na kwamba ataendelea kusalia nchini humo hadi pale yeyey mwenyewe atakapoamua kuondoka.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.