ZAMBIA-SIASA

Zambia; Hichilema asema hatambui uamuzi wa mahakama ya katiba

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema.
Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema. REUTERS/Rogan Ward

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema, ameeleza kusikitishwa na uamuzi wa mahakama ya katiba nchini humo, kutupilia mbali kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Mwishoni mwa juma, chama cha UPND kupitia mgombea wake, kiliwasilisha kesi katika mahakama ya katiba nchini humo, kikitaka mahakama hiyo ibatilishe matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi, Rais Edgar Lungu ambaye sasa ataapishwa juma lijalo.

Hakainde Hichilema ambaye alipoteza kwenye uchaguzi huo kwa kura laki moja, akidai kuwa kulikuwa na udanganyifu kwenye uchaguzi huo, ambapo alifungua kesi katika jitihada zake za kujaribu kumzuia Lungu asiendelee kukaa madarakani.

Baada ya uamuzi huo, Hichilema aliwaambia wanahabari kuwa, hakufurahishwa na hukumu ya mahakama ya katiba na kwamba vielelezo alivyokuwa ameviwasilisha mbele ya mahakama vilitosha kuwashawishi majaji wa mahakama hiyo kuipa uzito kesi yake.

Mwishoni mwa juma mahakama hiyohiyo ilimpa muda wa siku mbili zaidi Hichilema kuwasilisha kesi yake katika mahakama hiyo, lakini katika kile kilichoonekana ni hatua ya kushangaza, jaji Annie Sitali aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema mahakama hiyo haina kesi ya kusikiliza kupinga uchaguzi kwakuwa muda wa siku 14 uliotolewa kikatiba kupinga matokeo ulikuwa umepita.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa uamuzi wa mahakama hiyo ulitarajiwa kwakuwa tayari uchaguzi wenyewe uligubikwa na kasoro nyingi, huku ni wazi ikionekana kuwa Rais Lungu ana mkono wake katika vyombo vya sheria ambavyo haviwezi kwenda kinyume.

Wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na idhaa ya RFI Kiswahili, wamesema kuwa, kilichoamuliwa na mahakama kilitarajiwa kwakuwa nchi nyingi za Afrika, demokrasia haibugudhiwi tu peke yake wakati wa uchaguzi lakini pia hata kwenye mifumo ya kimahakama.

Baada ya hukumu hiyo chama cha UPND, kilitangaza rasmi kutotambua hukumu hiyo na kuutangazia uma wa Zambia kuwa hawakubaliani na maamuzi hayo.

Kwa uamuzi huu wa mahakama, Rais Edgar Lungu sasa ataapishwa rasmi kuendelea kuwa kiongozi wa taifa hilo, September 13.