GABON

Rais Bongo awatuhumu waangalizi wa umoja wa Ulaya

Rais mteule wa Gabon, Ali Bongo Ondimba, amewatuhumu waangalizi wa uchaguzi kutoka umoja wa Ulaya, ambao wameukosoa uchaguzi uliofanyika nchini mwake juma moja lililopita, wakidai ulikuwa na dosari na uonevu kwa mpinzani wake Jean Ping.

Rais Ali Bongo Ondimba katika mkutano na waandishi wa habari Septemba 1, 2016.
Rais Ali Bongo Ondimba katika mkutano na waandishi wa habari Septemba 1, 2016. AFP
Matangazo ya kibiashara

Jumanne ya September 6 mwaka huu, waangalizi wa umoja wa Ulaya walitoa tathmini ya ripoti ya waangalizi wake kwenye mji wa Haut-Ogooue, ambako ni ngome kuu ya Rais Bongo, ambapo wamesema kulikuwa na wizi mkubwa wa kura pamoja na kukiukwa kwa sheria na kanuni za uchaguzi.

Akizungumza kupitia kituo cha taifa cha Redio cha RTL, Rais Bongo amesema kuwa, angetamani kuona waangalizi hao pia wanagusia kasoro zilizoshuhudiwa kwenye ngome za mpinzani wake wake, mjini Fiefdom.

“Kama tunajaribu kuonesha dosari za uchaguzi, basi lazima tuwe wazi, tuzingatie usawa na kuainisha kasoro zote ambazo zimeripotiwa.” Alisema Rais Bongo.

Bongo ambaye yuko madarakani toka mwaka 2009, alidai kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa Agosti 27 mwaka huu, ambapo alimzidi mpinzani wake kwa karibu kura laki moja.

Upinzani nchini Gabon, umekataa kutambua matokeo ya kwenye mji wa Haut-Ogooue, ambako maofisa wa uchaguzi wamerekodi kujitokeza kwa idadi kubwa ya watu kuwahi kushuhudiwa, ambapo tume ya uchaguzi inasema, idadi hiyo ilikuwa zaidi ya asilimia 99, huku asilimia 95 wakimchagua Bongo.

Kwenye uchambuzi wao, waangalizi wa umoja wa Ulaya wamesema kuwa “idadi ya watu ambao hawakuwa halali kupiga kura ilikuwa kubwa huku baadhi ya karatasi zikiwa hazikuandikwa chochote zikihesabiwa kwenye mji wa Haut-Ogooue.”

Rais Bongo amekataa kutudiwa kuhesabiwa kwa kura zote nchi nzima, huku akidai kuwa ni mahakama ya katiba pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuagiza kura kuhesabiwa upya na kwamba hawezi kukiuka sheria za uchaguzi.

Bongo amejikuta kwenye shinikizo kubwa kutoka ndani na nje ya nchi yake baada ya kujiuzulu kwa waziri wake wa sheria, Seraphin Moundounga, ambaye wakati akijiuzulu alitaka kuhesabiwa kwa kura, kituo hadi kituo.