MAREKANI-SUDAN KUSINI

Washington yapinga kurudi kwa Machar serikalini

Kiongozi wa upinzani na aliye kuwa Makamu wa rais wa Sudan kusini Riek Machar, Julai 8, 2015.
Kiongozi wa upinzani na aliye kuwa Makamu wa rais wa Sudan kusini Riek Machar, Julai 8, 2015. REUTERS

Marekani imepinga kurudi kwa Riek Machar kwenye wadhifa wa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini. Mjumbe maalum wa Marekani nchini Sudan na Sudan Kusini, Donald Booth, katika taarifa yake ya Jumatano wiki hii, alitoa hoja hiyo mbele ya Baraza la wawakilishi la Congress mjini Washington.

Matangazo ya kibiashara

"Kutokana na kile kilichotokea, hatudhani kwamba itakuwa busara iwapo atarejeshwa kwenye nafasi yake katika serikali ya Juba," alisema Bw Booth mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje katika Baraza la Wawakilishi.

"Lakini hii haipaswi kutumika kama uhalali kwa Rais Salva Kiir kwa kuhodhi madaraka na kukandamiza wapinzani wake," alisema mwanadiplomasia huyo wa Marekani.

Kwa mujibu wa Donald Booth, Riek Machar na Salva Kiir, Rais wa Sudan kusini hawana nia njema ya kufanya kazi kwa pamoja katika utekelezaji wa mkataba wa amani uliyoafikiwa mwaka 2015.

Kiongozi wa waasi na rais wa Sudan Kusini hawataki kabisa kuzuia mapigano nchini Sudan Kusini, Bw Booth ameongeza.

Kwa mujibu wa Donald Both, watu hawa wawili wamepoteza udhibiti wa askari wao.

Riek Machar alikimbia kutoka Juba baada ya mapigano makali kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji wake, mapigano ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 200 mwezi Julai.

Bw Machar Alikimbilia katika mji wa Khartoum, mji mkuu wa nchi jirani ya Sudan.

Salva Kiir alimteua kwenye nafasi ya Makamu wa rais jenerali Taban Deng Gay, namba 2 wa kundi la waasi wa Riek Machar.