SOMALIA-IGAD

Viongozi wa IGAD kukutana mjini Mogadishu nchini Somalia

Mmoja wa mikutano iliyopita, iliyofanyika jijini Addis  Ababa nchini Ethiopia
Mmoja wa mikutano iliyopita, iliyofanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia theinsider.ug

Usalama umeimarishwa mjini Mogadishu nchini Somalia kuelekea mkutano wa marais kutoka Mataifa ya Afrika Mashariki IGAD, unaofanyika siku ya Jumanne.

Matangazo ya kibiashara

Mji wa Mogadishu kwa mara ya kwanza utawaleta pamoja viongozi kutoka Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda kujadili maswala mbalimbali.

Suala kubwa katika mkutano huu ni kuhusu hali ya usalama nchini Somalia lakini pia Uchaguzi wa wabunge na rais unaofanyika mwezi huu wa Septemba na Oktoba.

Hali ya usalama na siasa nchini Sudan Kusini pia ni suala litakalojadiliwa katika mkutano huo wa marais.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud amesisitiza kuwa pamoja na kwamba kundi la Al Shabab limeondolewa mjini Mogadishu, usalama umeimarishwa kila kona ya mji huo kwa sababu ya mashambulizi ya hivi karibuni katika mji huo.

Mara ya mwisho kwa Somalia kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu ilikuwa ni mwaka 1974, wakati ilipokuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa Afrika.

Wachambuzi wa maswala ya usalama wanasema hatua ya viongozi wa IGAD kukutana mjini Mogadishu ni kuonesha dunia kuwa vita dhidi ya Al Shabab vinazaa matunda na usalama unarejea nchini humo.