AFRIKA KUSINI

Afrika Kusini yakubali kuongezwa kwa ada ya vyuo vikuu, hofu ya maandamano yatanda

Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wakiwa kwenye moja ya maandamano ya mwaka jana kupinga kuongezwa kwa ada katika vyuo vikuu, Serikali sasa imekubali kuongezwa kwa ada.
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wakiwa kwenye moja ya maandamano ya mwaka jana kupinga kuongezwa kwa ada katika vyuo vikuu, Serikali sasa imekubali kuongezwa kwa ada. http://www.dailymaverick.co.za

Nchi ya Afrika Kusini Jumatatu ya wiki hii, imetoa kibali kwa vyuo vikuu nchini humo kuendelea mbele na mpango wao wa kuongeza ada za masomo kwa zaidi ya asilimia 8, wakati huu maandamano mapya yakitarajiwa.

Matangazo ya kibiashara

Mwaka jana, Serikali ilikabiliwa na maandamano makubwa ya nchi nzima yaliyofanywa na wanafunzi pamoja na wazazi kupinga uamuzi wa vyuo vikuu nchini humo kupandisha ada za masomo.

Mwaka 2015, vuguvugu la wanafunzi lilifanikiwa kutoongezewa kiasi chochote cha ada baada ya maandamano ya muda mrefu, ambapo walitaka pia kusitishwa mara moja kwa mipango yote ya upandishwaji wa ada katika vyuo vikuu, hadi pale kamati maalumu kuhusu fedha za vyuo vikuu kuketi na kutolea uamuzi suala hili.

Hata hivyo waziri wa elimu ya juu nchini Afrika Kusini, Bladr Nzimande, amewawashia taa ya kijani wamiliki wa vyuo vikuu nchini humo, kuongeza ada kwa mwaka wa fedha 2017.

“Vyuo vyetu vinakabiliwa na changamoto nyingi za kifedha” alisema waziri Nzimande ambaye alionesha wazi wazi kuwa, kuna haja ya ada hiyo kuongezwa ili vyuo hivyo viweze kujiendesha.

Waziri Nzimande, ameongeza kuwa “kutoongezwa ada kwa mwaka wa masomo wa 2016 ndio ambako kumechangia kwa kiasi kikubwa kushuhudiwa kwa changamoto hizi katika vyuo vikuu.”

Nzimande amependekeza vyuo vikuu vyote kuongeza ada zao lakini zisizidi asilimia 8 ambacho ndicho kiwango cha mwisho Serikali imeweka.

Mkuu wa chuo kikuu cha Cape Town, Max Price, amesema kuwa kushindwa kuongeza ada kutasababisha maelfu ya ajira kupunguzwa na kunguza msaada wa kifedha kwa wanafunzi masikini wanaosomeshwa na baadhi ya vyuo hivyo.

Serikali inasema kuwa yenyewe itagharamia nyongeza ya ada hiyo kwa wanafunzi ambao familia zao zinakipato cha chini ya Randi laki 6 kwa mwaka, sawa na dola za Marekani elfu 42.

Chuo kikuu cha Cape Town kilitangaza kusitisha masomo yake siku ya Jumatatu, siku ambayo waziri Nzimande ametoa tangazo la kukubali kuongezwa kwa ada huku Polisi ikiwanonya wanafunzi dhidi ya maandamano ya vurugu.