ZIMBABWE

Raia wa Zimbabwe kukabiliwa na kifungo jela ikiwa watatumia vibaya bendera ya taifa

Mchungaji Evan Mawarire, ambaye ameanzisha vuguvugu la kutumia bendera ya taifa kuupinga utawala wa Rais Mugabe.
Mchungaji Evan Mawarire, ambaye ameanzisha vuguvugu la kutumia bendera ya taifa kuupinga utawala wa Rais Mugabe. MUJAHID SAFODIEN / AFP

Raia na wanaharakati nchini Zimbabwe, sasa wanakabiliwa na kifungo gerezani, ikiwa watapatikana na hatia ya kuuza ama kutumia bendera ya taifa bila ya kuwa na kibali maalumu.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu wa Serikali umetangazwa na waziri wa sheria, ambaye amewaonya wananchi na wanaharakati nchini humo, kutotumia bendera ya taifa kiholela bila ya kuwa na kibali maalumu, hatua hii imekuja baada ya wanaharaka wanaodai mabadiliko nchinik humo, kuitumia bendera ya taifa kama ishara yao ya kudai mabadiliko na kuikosoa Serikali.

Waziri Virginia Mabhiza amesema kwenye taarifa yake kuwa, uma unataarifiwa kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kutumia bendera ya taifa bila ya kupata kibali maalumu kutoka Serikali, huku akisisitiza kuwa watakaokiuka agizo hili watakabiliwa na mkono wa Sheria.

Waziri Mabhiza amesema kuwa, mtu atakayepatikana na hatia, atakabiliwa na kifungo kisichozidi mwaka mmoja jela au kulipa faini ya dola za Marekani 200 au vyote kwa pamoja.

Bendera ya taifa ya Zimbabwe imekuwa ikitumiwa na wanaharakati kama nembo ya harakati zao za kudai mabadiliko na kuukosoa utawala wa Rais Robert Mugabe, ambapo kwa mara ya kwanza ilitumiwa kama nembo ya mabadiliko na mchungaji Evan Mawarire, ambaye aliweka picha za video kwenye mtandao akiwa ameiviringisha bendera hiyo shingoni mwake.

Serikali inasema kuwa, wamebaini katika siku za hivi karibuni, kuongezeka wimbi kubwa la wananchi kutumia bendera ya taifa katika shughuli ambazo haziko kikatiba.

Tangazo hili la Serikali limetolewa wakati huu, nchi hiyo ikishuhudia maandamano mfululizo yaliyoitishwa na upinzani pamoja na wanaharakati, wakiukosoa utawala wa Rais Mugabe, kwa kushindwa kudhibiti uchumi wataifa hilo na kusababisha hali mbaya kwa wananchi.

Waandamanaji pia wanashinikiza kufanyika marekebisho ya sheria ya uchaguzi, kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2018.

Kufuatia matumizi ya bendera ya taifa kama ishara na nambo ya harakati ya mabadiliko nchini humo, maelfu ya wamachinga na wafanyabiashara ndogondogo wamechepisha kwa uwing bendera hizo na kuziuza kwa waandamanaji.

Tayari wanaharakati na baadhi ya wanasiasa wamekosoa uamuzi huu wa Serikali, wakisema kuwa unalenga kuwanyima uhuru wananchi kutumia bendera ya nchi yao kuonesha utaifa.