DRC

Waratibu wa maandamano DRC kukamatwa, polisi yatoa takwimu za waliokufa

Polisi nchini DRC wakionekana wakilinda moja ya eneo ambalo hivi karibuni upinzani uliandaa maandamano.
Polisi nchini DRC wakionekana wakilinda moja ya eneo ambalo hivi karibuni upinzani uliandaa maandamano. REUTERS/Stringer

Polisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, imesema kuwa watu 32 ndio waliouawa wakati wa vurugu za siku mbili zilizotokana na maandamano yaliyokuwa yameitishwa na muungano wa vyama vya upinzani, kushinikiza Rais Josephu Kabila kuondoka madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Wakati Polisi mjini Kinshasa ikidai kuwa waliouawa ni 32 pekee huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, upinzani unasema idadi ya waliokufa kwenye maandamano hayo ni mara tatu ya idadi iliyotangazwa na Polisi.

Ripoti hii inatolewa wakati ambapo vyombo vya usalama vimefanikiwa kumaliza machafuko ya siku mbili ambayo yalianza kwa maandamano ya amani kabla ya baadae kugeuka na kuwa vurugu.

Makabiliano kati ya polisi na waandamanaji wa upinzani Jumatatu na Jumanne ya wiki hii, yalishuhudia watu wakichomwa moto wakiwa hai, kushambuliwa kwa vituo vya polisi huku makabiliano haya yakiwa ni mabaya zaidi kwenye jiji la Kinshasa toka yale ya mwezi January 2015.

Msemaji wa jeshi la Polisi, Pierre-Rombaut Mwana-Mputu, amewaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wakisaidiwa na wanajeshi, walifanikiwa kuzuia uhalifu na uporaji uliokuwa ukifanywa na makundi ya vijana wa upinzani.

Hali ya foleni haikushuhudiwa kabisa Jumatano ya wiki hii kwenye jiji la Kinshasa ambalo ni maarufu kwakuwa na msongamano wa magari na watu, huku wananfunzi wengie wakiendelea kusalia majumbani mwao kwa hofu ya kiusalama.

Idadi rasmi ya waliokufa ni chini na ile iliyotolewa na upinzani ambao unadai ni watu 100 waliokufa, huku ile idadi ya polisi ikielekea kufanana na ile iliyotolewa na shirika la Human Right Watch lililodai ni watu 37 ndio waliokufa.

Hata hivyo, umoja wa Mataifa wenyewe ambao una vikosi vyake vya kulinda amani mashariki mwa nchi hiyo, haujataka kusema idadi kamili ya watu waliokufa kwenye machafuko hayo.

Jumatano ya wiki hii, baraza la usalama la umoja wa Mataifa limetoa wito wa kudumishwa amani na kuwataka wanasiasa na raia kujiepusha na vurugu huku likitaka kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Katika hatua nyingine, mwendesha mashtaka wa Serikali ametoa kibali kwa jeshi la polisi nchini humo, kuwakamata vinara walioratibu maandamano ya mwanzoni mwa juma hili ikiwa ni pamoja na kuwazuia kutoka nje ya nchi.