GABON-SIASA

Jean Ping asema mahakama haikutenda haki kumpa ushindi Ali Bongo

Kiongozi wa upinzani nchini Gabon Jean Ping ameelezea kutoridhishwa na maamuzi ya mahakama ya kikatiba ambayo ilihalalisha ushindi wa Ali Bongo kuwa raisi wa nchi hiyo.

Mahakama ya Katiba ya Gabon
Mahakama ya Katiba ya Gabon © (Photo : AFP)
Matangazo ya kibiashara

Jean Ping aliwasilisha kesi Mahakamani kutaka kura kuhesabiwa upya kwa madai kuwa, aliibiwa kura  madai ambayo Majaji wa Mahakama hiyo wameyatupilia mbali.

Ping ameituhumu mahakama kupendelea na kutotenda haki kufuatia maamuzi ya mapema jumamosi kwamba Ali Bongo ndie mshindi wa kura halali za uchaguzi wa August 27.

Uamuzi huo ulitolewa, huku hali ya wasiwasi ikitanda katika jiji kuu Libreville kwa hofu kuwa huenda kukatokea makabiliano makali kati ya polisi na wafuasi wa Ping.

Polisi wanaonekana  wakipiga doria katika jiji hilo wakiwa wamejihami tayari kukabiliana na wafuasi wa upinzani.

Watu wakiwa kwenye foleni kutoa pesa Benki jijini Libreville
Watu wakiwa kwenye foleni kutoa pesa Benki jijini Libreville AFP

Siku ya Ijumaa, watu walionekana wakinunua vyakula, huku foleni ndefu zikishuhudiwa katika benki mbalimbali kwa hofu kuwa hali itakuwa mbaya kuanzia siku ya Jumamosi.

Rais Bongo amelihotubia taifa baada ya uamuzi huo wa Mahakama na kutaka kuwepo kwa mazungumzo ya kisiasa kati ya serikali na upinzani.

Aidha, ameonya kuwa ikiwa kutakuwa na fujo, serikali itamkamata Jean Ping ili kumwajibisha.

Rais Ali Bongo (Kulia) na mpinzani wake Jean Ping (Kushoto)
Rais Ali Bongo (Kulia) na mpinzani wake Jean Ping (Kushoto) icibrazza.com

Mahakama hiyo imesema rais Bongo alishinda uchaguzi huo kwa ushindi wa asilimia 50.66 huku Ping akiwa wa pili kwa kupata asilimia  47.24.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, ametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kuwa watulivu baada ya uamuzi huu wa Mahakama.

Profesa Larry Gumbe mchambuzi wa siasa barani Afrika kutoka jijini Nairobi nchini Kenya akihojiwa na RFI Kiswahili, amesema uamuzi kama huu ulitarajiwa na njia mwafaka ya kuleta utulivu wa kisiasa nchini humo ni rais Bongo na Ping kuingia katika serikali ya muungano.