GABON-SIASA

Kiongozi wa upinzani nchini Gabon akataa uamuzi wa Mahakama ya kikatiba

Kiongozi wa upinzani nchini Gabon Jean Ping amesema hawezi kutambua uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba kuwa, rais Ali Bongo alishinda Uchaguzi wa urais mwezi uliopita.

Kiongozi wa upinzani nchini Gabon Jean Ping
Kiongozi wa upinzani nchini Gabon Jean Ping afriqueinside.com
Matangazo ya kibiashara

Ping amesisitiza kuwa yeye ndiye aliyeshinda Uchaguzi huo na kuongeza kuwa atahakikisha kuwa haki ya wale wote waliompigia kura kuwa rais, inaheshimiwa.

Kuhusu uamuzi wa Mahakama, Ping amesema uliegemea upande mmoja.

Kauli hii ya Ping inazua hali ya wasiwasi nchini humo, wakati huu jiji kuu la Libreville likiendelea kudhibitiwa na maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia.

Mahakama siku ya Ijumaa, iliamua kuwa rais Bongo alishinda Uchaguzi huo kwa kupata asilimia 50 huku mpinzani wake akipata asilimia 47.

Majaji wa Mahakama hiyo walikataa kupokea ushahidi wa Ping kwa kile walichokieleza kuwa, mawakili wake walishindwa kuthibitisha kuwa ulikuwa sahihi.

Rais Bongo, ametaka kuwepo kwa mazungumzo ya kisiasa nchini humo baada ya uamuzi huo wa Mahakama na kuonya kuwa Ping atakamatwa ikiwa kutakuwa na fujo.

Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo Emmanuel Isozet Ngondet akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani, ameiomba Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia nchi yake kurejesha umoja wa kitaifa baada ya Uchaguzi wa mwezi uliopita.