GABON-SIASA

Ali Bongo aapishwa, aahidi kuwatumikia raia wote wa Gabon

Rais wa Gabon Ali Bongo ameapishwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine baada ya Mahakama ya Kikatiba kuamua wiki iliyopita kuwa alishinda kihalali.

Ali Bongo akiapa kuiongoza Gabon
Ali Bongo akiapa kuiongoza Gabon dailymail.co.uk
Matangazo ya kibiashara

Bongo ameahidi kutumia nguvu zake zote kwa maslahi ya wananchi wa Gabon, kuilinda na kutoheshimu katiba ya nchi hiyo.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 57, ameapishwa Ikulu katika jiji kuu Libreville chini ya ulinzi mkali.

Sherehe za kumwapisha rais Bongo, zimehudhuriwa na viongozi wa kutoka Mali, Niger, Togo na Sao Tome.

Mataifa mengine yaliyowakilishwa katika sherehe hiyo ni Chad, Senegal, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Morocco yaliyowakilishwa na Mawaziri wakuu na wawakilishi wengine.

Kiongozi huyo ameapishwa wakati huu taifa hilo likisalia kugawanyika kisiasa baada ya Jean Ping aliyewania wadhifa huo akiendelea kusisitiza kuwa yeye ndiye aliyeshinda.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, rais Bongo alitoa wito wa kufanyika kwa  mazungumzo ya kisiasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo ambao waangalizi wa Umoja wa Ulaya walidai kuwa haikuwa wazi.