ETHIOPIA

Serikali ya Ethiopia yakanusha wanajeshi kutumia risasi dhidi ya raia, watu 52 wamekufa

Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.
Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn. youtube.com

Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, amekanusha madai kuwa vikosi vya nchi yake vilivyatua risasi kuwatawanya mamia ya waandamanaji na raia waliohudhuria sherehe za kumalizika kwa msimu wa mvua nchini humo na badala yake amewalaumu wanaharakati wanaopigania demokrasia.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya waziri mkuu Desalegn imekuja wakati huu Serikali ikithibitisha vifo vya watu 52 ambao walipoteza maisha kwa kukanyagana wakati wakikimbia baada ya polisi kuwafyatulia risasi na mabomu ya machozi.

Vurugu hizi zilitokea kwenye mji wa Bishoftu jirani na jiji kuu la Ethiopia, Addis Ababa, ambako wazee wa kimila kutoka kwenye mji wa Oromo walikuwa wakifanya sherehe za kutamatika kumalizika kwa msimu wa mvua nchini humo.

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji ambao walijichanganya katikati ya sherehe hizo na kuanza kuimba nyimbo za kuikashifu Serikali kwa kuminya demokrasia, pamoja na kupinga mpango wa Serikali yao kutaka kupanua jiji la Addis Ababa hadi kwenye mji wa Oromo.

Hata hivyo wapinzani wamepinga idadi ya vifo iliyotolewa na Serikali, wakisema kuwa watu waliofariki wanazidi 100.

Haya yanajiri wakati huu nchi hiyo ikishuhudia maandamano makubwa ya kuipinga Serikali ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini humo kwa miongo kadhaa.