CITES-WANYAMAPORI

Mataifa yaridhia sheria kali zaidi kuwalinda wanyama walioko hatarini kutoweka

Tembo wa Afrika ambao wamekubaliwa kulindwa kwa nguvu zote.
Tembo wa Afrika ambao wamekubaliwa kulindwa kwa nguvu zote. http://www.ictsd.org

Mkutano wa kidunia kuhusu biashara ya wanyama pori, umetamatika jijini Johannesburg, Afrika Kusini, huku wajumbe wa mkutano huo wakiridhia na kufanya maamuzi kuhusu namna bora ya kukabiliana na biashara haramu ya bidhaa na wanyama walioko hatarini kutoweka duniani.

Matangazo ya kibiashara

Maofisa wa Serikali na wanaharakati wa masuala ya mazingira waliokutana chini ya mwavuli wa kongamano la kimataifa kuhusu biashara ya wanyama walioko hatarini kutoweka, wamekubaliana kwa kauli moja kupitisha sheria kali zaidi kudhibiti biashara hiyo.

Mijadala mikali iliibuka kwenye mkutano huo na wakati fulani kuonekana mgawanyiko mkubwa baina ya wajumbe, ambapo nchi za Afrika ziliyatuhumu mataifa ya magharibi kwa kujaribu kuwaelekeza nini cha kufanya kuwalinda tembo wao.

Wanaharakati wa mazingira duniani wamepongeza yale yaliyoridhiwa kwenye mkutano huo, ambapo wameunga mkono sheria zilizoridhiwa na wajumbe wa mkutano huo, ambao wamesema zitasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda mimea na wanyama walioko hatarini kutoweka.

Muungano wa nchi 29 zikiongozwa na Kenya na Benin, zimeshinikiza tembo wa Afrika kuwekwa kwenye orodha ya wanyama wanaolindwa zaidi na kupiga marufuku kabisa biashara ya pembe za ndovu.

Hata hivyo nchi za Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe zilipinga maazimio haya mapya, ambapo awali zilitaka ziruhusiwe kuuza shehena ya pembe za ndovu na faru inazozishikilia.