ZAMBIA

Hichilema na makamu wake wakamatwa, washtakiwa kwa makosa ya uchochezi

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchinij Zambia, Hakainde Hichilema, pamoja na naibu kiongozi wa chama hicho, hii leo wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za uchochezi baada ya kukamatwa na polisi Jumatano ya wiki hii.

Hakainde Hichilema, kinara wa chama kikuu cha upinzani nchini Zambia cha UPND.
Hakainde Hichilema, kinara wa chama kikuu cha upinzani nchini Zambia cha UPND. REUTERS/Rogan Ward
Matangazo ya kibiashara

Hichilema, ambaye anapinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyomrejesha madarakani rais Edgar Lungu kwenye uchaguzi wa mwezi Agosti mwaka huu, alizuiliwa na polisi akiwa sambamba na Geoffrey Mwamba, makamu wa rais wa chama chake cha UPND.

Mkuu wa jeshi la polisi kwenye mkoa wa Copperbelt, Charity Katanga, amethibitisha kukamatwa kwa viongozi hao wawili, ambapo amesema wamehojiwa kwa makosa ya uchochezi na kufanya mikutano ya kuhamasisha vurugu.

Polisi kwenye mji huo, imedai kuwa Hichilema na makamu wake, walifanya mkutano september 26 mwaka huu kwenye mji wa Mpongwe, kinyume cha Sheria, ambapo wanadaiwa kuwa walitoa matamshi ya uchochezi dhidi ya Serikali na kuhamasisha vurugu.

Kukamatwa kwao kumekuja ikiwa ni wiki moja tu imepita, toka wazuiliwe na polisi kuwatembelea gerezani wafuasi wao waliokamatwa wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi, ambapo baadae waliamua kwenda kusalimia familia zao.

Hichilema anamtuhumu rais Lungu, tume ya uchaguzi na majaji wa mahakama kuu nchini humo kwa kuwa washirika wa njama zilizoharibu uchaguzi wa Agosti 11, ambapo Lungu alishinda kwa toauti ya kura laki 1.