TUTU-AFRIKA KUSINI

Askofu Desmond Tutu aomba haki ya kusaidiwa kufa

Mwanaharakatik aliyepinga vitendo na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu, ametangaza kuwa anaomba haki ya kuchagua kusaidiwa kufa.

Mshindi wa tuzo ya Nobel na mwanaharakati wa ubaguzi wa rangi, Askofu Desmond Tutu, raia wa Afrika Kusini ambaye ameomba kusaidiwa kufa.
Mshindi wa tuzo ya Nobel na mwanaharakati wa ubaguzi wa rangi, Askofu Desmond Tutu, raia wa Afrika Kusini ambaye ameomba kusaidiwa kufa. UN Photo/Paulo Filgueiras
Matangazo ya kibiashara

Askofu Tutu ambaye ni mshindi wa tuzo la Nobel, amesema kuwa, asingependa kuendelea kuwekwa hai kwa gharama yoyote ile, Tutu ameyasema haya kwenye barua yake aliyoiandika kwenye gaezti la Washington Post.

Kauli yake imewakumbusha watu kuhusu harakati aliyoifanya mwaka 2014, ambapo aliongoza kampeni ya kuomba watu waruhusiwe kuchagua kusaidiwa kufa bila ya kuweka wazi ikiwa yeye mwenyewe siku moja angeomba kufanya hivyo.

Askofu Tutu alilazwa hospitalini mwezi uliopita ambapo alikuwa anasumbuliwa na maambukizi ya kwenye kidonda chake alichowahi kufanyiwa operesheni.

“Ni matumaini yangu kuwa nathaminiwa na nitaruhusiwa kufa kwenda kwenye maisha mengine kwa uchaguzi wangu mimi,” aliandika Askofu Tutu.

“Bila ya kujali kile utakachoenda kukichagua, kwanini uwakatalie wengine kufanya uchaguzi wao binafsi? Aliuliza.

Mpaka sasa nchi ya Afrika Kusini haina sheria inayoruhusu mtu kusaidiwa kufa ikiwa atachagua kufanya hivyo kwa matakwa yake.

Lakini katika uamuzi wa aina yake mwezi April mwaka 2015, mahakama moja nchini Afrika Kusini iliruhusu kwa raia mmoja kusaidiwa kufa, hali iliyoibusha mjadala mkali kutaka ufafanuzi wa sheria hiyo.