ZIMBABWE

Mugabe atangaza mpango wa kulegeza masharti ya sheria ya ardhi ya mwaka 2008

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe.
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe. Reuters/Philimon Bulawayo

Rais wa Zimbabwe, Robert MUGABE, juma hili ametangaza kuwa, anapanga kulegeza masharti ya sera yake ya umiliki wa ardhi kwa wazawa, ambapo sasa makampuni ya kigeni yanalazimika kugawana sehemu ya ardhi yake na wawekezaji wa ndani.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa bunge la nchi hiyo, rais Mugabe aliwaambia wanasiasa kuwa, Serikali imeanza kupitia upya Sera yake ya kurasimisha radhi kutoka kwa wageni, ili kuvutia wawekezaji.

Kauli yake imekuja ikiwa ni miezi michache tu imepita, ambapo mwezi Marchi mwaka huu, Serikali ilitishia kuyafunga makampuni yote ya kigeni nchini humo ambayo yatakuwa yameshindwa kutekeleza sheria ya ardhi iliyopitishwa mwaka 2008.

Hata wiki chache baadae rais Mugabe alijaribu kuwahakikishia wawekezaji wa kigeni kuwa, sekta nyingine kama benki zitakuwa hazihusiki na zisingeguswa na sheria hii ambayo wataalamu wa masuala ya uchumo wanaikosoa kwa kuwa imezuia uwekezaji wa kigeni kwenye taifa hilo.

Serikali inasema kuwa sheria hiyo, ilikuwa na lengo la kuwanufaisha wazawa ambao waliminywa na kunyang’anywa ardhi wakati wa ukoloni, lakini wakosoaji wa Serikali wanasema sheria hiyo imewanufaisha zaidi washirika wa rais Mugabe.

Uamuzi wa rais Mugabe unatazamwa na upinzani kama njama ya kiongozi wao kutaka kuwashawishi wananchi wasiandamane kupinga hali mbaya ya uchumi inayoikabili nchi yao.