ETHIOPIA-USALAMA

Hali ya hatari yatangazwa Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Januari 26, 2013.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Januari 26, 2013. REUTERS/Tiksa Negeri

Serikali ya Ethiopia imetangaza hali ya hatari, kwa kipindi cha miezi sita, kufuatia miezi kadhaa ya machafuko na vurugu nchini. Vikosi vya usalama vimekua vikinyooshewa kidole kuhusika na vitendo vingi viovu.

Matangazo ya kibiashara

"Hali ya hatari imetangazwa baada ya majadiliano ya kina katika Baraza la Mawaziri kuhusu watu waliopoteza maisha na uharibifu wa mali vilivyotokea nchini," amesema Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn.

"Hatutovunja uhuru wa kidemokrasia. Kuna haki tunazopewa na Katiba. Haki hizi haziwezi kubadilishwa na mtu yeyote, hata serikali haina uwezo huo, hata wakati wa hali ya hatari," Waziri wa Habari wa Ethiopia, Getachew Reda amebainisha.

"Lakini kama vikosi vya usalama vinaona kuwa mafanikio ya malengo yao yanahitaji kupiga marufuku shughuli fulani (...) serikali haiwezi kupinga," Bw. Reda amesema.

Ethiopia kwa sasa inakabiliwa na maandamano makubwa dhidi ya serikali kwa miaka 25.

Maandamano yaliyovunjwa na vikosi vya usalama tangu mwishoni mwa mwaka 2015 yalisababisha mamia ya watu kupoteza maisha, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu.

Maandamano haya yanaongozwa na jamii za Oromo na Amhara.

jamii hizi ambazo zina watu wengi zinabaini kwamba zinatengwa na serikali.