AFRIKA KUSINI

Ulinzi waimarishwa kwenye vyuo vikuu nchini Afrika Kusini

Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Afrika Kusini wakikabiliana na Polisi, wanapinga kuongezwa kwa ada za vyuo vikuu.
Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Afrika Kusini wakikabiliana na Polisi, wanapinga kuongezwa kwa ada za vyuo vikuu. DR

Ulinzi umeimarishwa kwenye vyuo vikuu kadhaa nchini Afrika Kusini, kufuatia maandamano na vurugu mfululizo za wanafunzi wanaoshinikiza kupunguzwa kwa ada za vyuo vikuu nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Polisi wa kutuliza ghasia Jumatatu ya October 10, wameshuhudiwa nje ya kampasi ya chuo kikuu cha Wits Braamfontein, huku kikundi cha wanafunzi wenye mabango kikionekana kuzingira chuo hicho.

Wanafunzi waliokusanyika nje ya chuo kikuu hicho na vyuo vingine wanaimba nyimbo za ukombozi.

Uongozi wa chuo hicho umetoa taarifa mwishoni mwa juma kueleza kuwa masomo yataendelea kama kawaida siku ya Jumatatu, lakini hata hivyo kiongozi wa wanafunzi kwenye chuol hicho, Mcebo Dlamini, amesema hawataingia darasano hadi pale madai yao ya elimu bure yatakapotekelezwa.

Ulinzi pia umeimarishwa kwenye vyuo vikuu vingine nchi nzima kutokana na hofu ya kutokea vurugu, kwa kile ambacho wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Afrika Kusini wanaendelea kushinikiza kusoma bure.

Kwa takriban majuma kadhaa sasa polisi nchini humo wamekuwa wakikabiliana na mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini humo, ambao wamekuwa wakifanya fujo nje ya vyuo vyao wakishinikiza madai yao kutekelezwa.

Vurugu hizi zimeanza baada ya tangazo la Serikali kuhusu kukubaliana na ombi la vyuo vikuu nchini humo kuongeza ada ya masomo kukabiliana na changamoto za kiuendeshaji, uamuzi ambao umepingwa vikali na wanafunzi.

Serikali kupitia wizara ya elimu ya juu nchini humo, inasisitiza kuwa nyongeza hiyo ni lazima hasa wakati huuu vyuo vingi vikikabiliwa na changamoto za kiutendaji kutokana na uhaba wa fedha, huku ikiahidi kuendelea kwasomesha wanafunzi wanaotoka kwenye mazingira magumu.