ETHIOPIA-UJERUMANI

Waziri mkuu wa Ethiopia asema yuko tayari kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi

Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.
Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn. REUTERS/Tiksa Negeri

Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn amesema kuwa, Serikali yake inataka kufanyia mabadiliko mfumo wa uchaguzi nchini humo, ambao uliwatenga wanasiasa wa upinzani na kusababisha mfululizo wa maandamano yaliyodumu kwa miezi kadhaa hivi sasa.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari wakati wa mkutano wake na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliyeko ziarani nchini humo, waziri mkuu Desalegn amesema kuwa, mfumo wa uchaguzi uliopo sasa unaruhusu mshindi kupata asilimia 51 ya kura zote na kumuwezesha kushinda viti vyote.

Waziri mkuu Desalegn ameongeza kuwa mabadiliko haya yanalenga kuwapa watu nafasi zaidi ya kupaza sauti zao hasa kwa wale ambao hawana uwakilishi ili wasikike bungeni.

Kwa mfumo uliopo sasa, chama tawala cha waziri mkuu Hailemariam Desalegn kinaumiliki wa viti vyote katika bunge la kitaifa lenye nafasi 546.

Kansela Merkel kwa upande wake amemwambia waziri mkuu Desalegn kuwa, demokrasia ya kweli ni pamoja na kuruhusu upinzani na Serikali kukubali kukosolewana sauti za watu wengi zaidi kusikika bungeni.

Kauli ya waziri mkuu Hailemariam Desalegn imekuja wakati huu Serikali yake ikiwa imetangaza hali ya darura kutokana na maandamano mfululizo ambayo mpaka sasa yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 50.