UN-DRC

UN yaonya kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko ya kisiasa nchini DRC

Maman S. Sidikou, mjumbe maalumu wa katibu mkuu na mkuu wa tume ya MONUSCO nchini DRC.
Maman S. Sidikou, mjumbe maalumu wa katibu mkuu na mkuu wa tume ya MONUSCO nchini DRC. UN Photo/Kim Haughton

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, mzozo wa kisiasa kuhusu Rais Josephu Kabila na jaribio lake la kutaka kuendelea kusalia madarakani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huenda kukasababusha machafuko zaidi ya kisiasa.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa unasema kuwa, nchi ya DRC imeingia kwenye kipindi cha hatari zaidi na kwamba hadi sasa hakuna jambo lolote lililochanya linalojionesha ikiwa nchi hiyo itaepuka sintofahamu ya kisiasa inayoinyemelea nchi hiyo.

Mjumbe wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa, Maman Sambo Sidikou, amewaambia wajumbe wa baraza hilo kuwa, pande zote mbili kila uchao zinaonesha ni ya kuwa tayari kuwa na mazungumzo ya kumaliza tofauti zao, lakini bado mazungumzo yanayoendelea yanakumbwa na dosari nyingi.

Sidikou, ameongeza kuwa, ikiwa suluhu ya kisiasa haitapatikana mapema, na namna ambavyo hali inaendelea kujitokeza kila siku, basi uwezekano wa kutokea machafuko ni mkubwa zaidi kuliko muda ambao jumuiya ya kimataifa itatumia kudhibiti.

Mwezi September mwaka huu, Polisi nchini DRC walikabiliana vikali na maelfu ya waandamanaji wa upinzani jijini Kinshasa, ambao walikuwa wakishinikiza kuondoka madarakani kwa Rais Josephu Kabila wakati muhula wake utakapotamatika.

Waandamanaji wa upinzani nchini DRC wakiwa kwenye barabara za jiji la Kinshasa.
Waandamanaji wa upinzani nchini DRC wakiwa kwenye barabara za jiji la Kinshasa. DR

Katika maandamano hayo, watu zaidi ya 37 walipoteza maisha ambapo baadhi ya mashirika ya kiraia na yale ya haki za binadamu yanasema idadi hiyo iliyotolewa na Serikali huenda ikawa imezidi kutokana na namna ambavyo makabiliano yalikuwa.

Tume ya umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO imeorodhesha baadhi ya matukio ya mauaji yaliyofanyika nchini humo na kuyahusisha na askari maalumu wa rais Josephu Kabila ambao wamekuwa wakitumiwa kuwaua raia.

Sidikou ambaye anaongoza tume ya umoja wa Mataifa nchini DRC yenye wanajeshi elfu 22, ameonya kuwa walinda amani wa umoja huo huenda wasiwe na uwezo wa kudhibiti machafuko ya kisiasa yatakayojitokeza ikiwa suluhu haitapatikana mapema.

Mjumbe huyo ameongeza kuwa MONUSCO itaendelea kutoa msaada na ulinzi kwa raia wa DRC, lakini itakuwa vigumu sana kwa tume yake kuwalinda raia wote kwa wakati mmoja wakati vurugu zitakapoteokea.

Baadhi ya vijana wakiwa wamechoma matairi kwenye moja ya barabara za Kinshasa
Baadhi ya vijana wakiwa wamechoma matairi kwenye moja ya barabara za Kinshasa https://cdn-images

Wakati huu maandamano mapya yakiwa yameitishwa October 19 mwaka huu, Sidikou ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza bidii kuzishawishi pande zinazokinzana nchini DRC kuendelea na mazungumzo ili kupata muafaka utakaoinusuru nchi hiyo na kutumbukia kwenye vurugu za kisiasa.

Upinzani unamtuhumu rais Kabila ambaye yuko madarakani toka mwaka 2001, kwa kujaribu kubadili mfumo wa uchaguzi ili aendelee kusalia madarakani wakati muhula wake wa pili na wa mwisho utakapokuwa unatamatika December 20 mwaka huu.