LIBYA-USALAMA

Utata waibuka katika jeshi la Libya

Jeneral Khalifa Haftar katika mji wa Abyar, mashariki mwa mji wa Benghazi, Mei 31 mwaka 2014.
Jeneral Khalifa Haftar katika mji wa Abyar, mashariki mwa mji wa Benghazi, Mei 31 mwaka 2014. REUTERS/Esam Omran Al-Fetori

Wito kwa umoja wa jeshi la Libya umeendelea kuongezeka, wito wa hivi karibuni ni ule wa mjini Niamey, Jumatano, Oktoba 19, baada ya mkutano wa nchi jirani za Libya. Hata hivyo utata mpya umeibuka katika jeshi la Libya mjini Tripoli. Taarifa ya mwisho baada ya mkutano wa kundi la maafisa kutoka magharibi mwa Libya imemtaja Afisa mkuu wa jeshi Khalifa Haftar kuwa amehusika na 'mapinduzi na uhalifu wa kivita.'

Matangazo ya kibiashara

Tayari mgawanyiko umeanza kujitokea katika jeshi la libya, wakati ambako jumuiya ya kimataifa imekua ikitoa wito wa kuunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa miezi ya hivi karibuni.

Kauli hii, ya 'kiongozi wa mapinduzi na uhalifu wa kivita, imekuwa ikitumiwa na wapiganaji wa kiislamu nchini Libya kwa kumchafua Khalifa Haftar. Kwa miaka miwili na nusu, afisa huyo wa ngazi ya juu katika jeshi la Libya amekua akiongoza vita dhidi ya makundi ya wapiganaji wa kiislamu katika miji kadhaa mashariki mwa Libya. Tayari hali hii inaonyesha kuwa miongoni mwa maafisa wa jeshi kutoka magharibi kuna wale wana uhusiano na makundi ya wapiganaji wa kiislamu.

Maneno yao yaliweza kuingizwa katika taarifa ya mwisho ya mkutano, mkutano ambao kwa mujibu wa vyanzo vya RFI ulifanyika katika huku wajumbe wa makundi ya waasi wakiwepo. Taarifa ya mwisho, iliyosomwa, ilirushwa moja kwa moja kwenye runinga mbalimbali nchini Libya. Taarifa hii iliibua hali ya sintofahamu kati ya maafisa walioshiriki katika mkutano huo. Wengi hawakukubaliana na yaliyokuwemo katika tangazo hilo. Lakini wakati huo huo, Sadek Al-Ghiryani, kiongozi wa kiroho wa makundi kadhaa ya wapiganaji wa kiislamu wenye msimamo mkali, alikuwa katika kituo cha televisheni akimshutumu Khalifa Haftar kuwa ni "mtoto aliedekezwa na afisa wa jumuiya ya kimataifa. " Bw Al-Ghiryani amesema jumuiya ya kimataifa inamuandaa Haftar kumrithi Gaddafi.