CAMEROON-AJALI

Cameroon: idadi ya watu waliopoteza maisha yafikia 79

Nchini Cameroon, abiria waondolewa katika gari ya moshi iliyofanya ajali katika eneo la Esaka Oktoba 21, 2016
Nchini Cameroon, abiria waondolewa katika gari ya moshi iliyofanya ajali katika eneo la Esaka Oktoba 21, 2016 AFP/STRINGER

Watu Sabini na tisa ndio walipoteza maisha katika ajali ya gari moshi iliyotokea mjini Yaounde-Douala, nchini Cameroon Ijumaa wiki iliyopita, kulingana na idadi mpya iliyotolewa Jumatatu na redio ya serikali (CRTV).

Matangazo ya kibiashara

Jumapili Oktoba 23, zaidi ya miili 11 iliondolewa katika vifusi, na kupelekea idadi hiyo kufikia 79 jumla ya idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo,redio ya serikali (CRTV) imearifu, ikinukuu Wizara ya Afya. Radio imeongeza kuwa majeruhi 551 waliorodheshwa, ambapo wengi walisafirishwa katika mji wa Douala.

"Utafiti katika eneo la ajali ulikamilika Jumapili," afisa wa shirika la usafiri wa reli la Camrail ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la AFP. Jumamosi, afisa wa shirika la usafiri wa reli la Camrail alisema kuwa miili kati ya 60 na 70 ilisafirishwa katika mji wa Yaounde.

Kwa amri ya Rais Paul Biya, aliyerejea nchini Cameroon Jumapili hii baada ya mwezi mmoja akiwa nje ya nchi, serikali imetangaza maombolezo ya kitaifa kwa siku ya leo Jumatatu na bendera zimepandishwa nusu mlingoti. Kanisa Katoliki limetoa wito wa ibada kwa ajili ya wahanga wa ajali hiyo nchini kote.

"Nadhani (maombolezo ya kitaifa) ni njia bora ya kusisitiza mshikamano wa taifa nzima na waathirika wa janga hili?", Bw Biya alisema muda mfupi baada ya kuwasili kwake. "Nimeamuru uchunguzi uanzishwe, uchunguzi wa kina ili kujua chanzo cha ajali hii, " Rais Paul Biya alisisitiza.