IVORY COAST

Wananchi wa Ivory Coast wapigia kura ya ndio au hapana kuhusu katiba mpya

Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, wakati akipiga kura kuidhinisha mabadiliko ya katiba mpya ya nchi hiyo,  October 30, 2016.
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, wakati akipiga kura kuidhinisha mabadiliko ya katiba mpya ya nchi hiyo, October 30, 2016. REUTERS/Luc Gnago

Raia nchini Ivory Coast hii leo wamepiga kura ya kuamua kuidhinisha mabadiliko ya katiba mpya au la, kura ambayo Rais wa nchi hiyo, Alassane Ouattara, anasema itasaidia kumaliza miaka kadhaa ya uhasama na sintofahamu ya kisiasa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Hata hiyo wadadisi wa mambo wanasema kuwa, mabadiliko haya ya katiba yanayopigiwa kura na watu zaidi ya milioni 6 na laki 3, yamewagawa upinzani pamoja na baadhi ya wapiga kura.

Vyombo vya habari nchini Ivory Coast, vimeripoti kuhusu kujitokeza kwa idadi ndogo ya watu kwenda kupigia kura katiba mpya, kwa kile ambacho wataalamu wanasema huenda mabadiliko hayo yasiungwe mkono.

Miongoni mwa mabadiliko yaliyoingizwa kwenye katiba hii mpya inayoungwa mkono na Ouattara, ni pamoja na kuanzishwa kwa nafasi ya makamu wa rais atakayechaguliwa na Rais pamoja na kuanzishwa kwa baraza la Seneti.

Mabadiliko mengine yanahusu kipengele cha uhalali wa mgombea urais nchini humo, ambapo kwa mujibu wa katiba iliyopo, rais ni lazima awe amezaliwa kutokana na wazazi waliozaliwa wote nchini Ivory Coast, kipengele ambacho sasa kitafanyiwa mabadiliko.

Suala hili ndilo ambalo lilichangia miaka kadhaa ya machafuko nchini humo, yakiwemo mapinduzi ya mwaka 1999 na vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002 ambavyo viliigawa nchi hiyo kati ya watu wa kaskazini na kusini na kisha vurugu za mara baada ya uchaguzi mwaka 2010.

Rais Ouattara ambaye ni maarufu katikati ya nchi hiyo, alizaliwa na baba mwenye asili ya Burkina Faso, suala ambalo liliibua mjadala ikiwa ataruhusiwa kuwania urais kwenye uchaguzi ujao.

Hata hivyo alifanikiwa kuvuka kiunzi hicho baada ya jumuiya ya kimataifa kuingilia kati siasa za nchi hiyo na kumlazimisha aliyekuwa rais wakati huo, Laurent Gbagbo kutia saini mkataba ulioruhusu raia yeyote wa nchi hiyo kuwania urais.

Kabla ya kura hii kufanyika, kulifuatia maandamano mfululizo ya wananchi wanaopinga mabadiliko yaliyopendekezwa kwenye katiba mpya.