UFARANSA-CAR

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa yuko Afrika ya Kati, kutamatisha operesheni Sangaris

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian. REUTERS/Charles Platiau

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian Jumapili hii amesafiri kuelekea nchini Jamhuri ya Kati, kutamatisha rasmi operesheni Sangaris inayotekelezwa na vikosi vyake toka miaka mitatu iliyopita, kikosi kilichotumwa kwa lengo la kudhibiti mauaji lakini kimeshindwa kuwanyang'anya silaha makundi ya wapiganaji.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe rasmi ya kutamatika kwa operesheni Sangaris ya Ufaransa, zitafanyika wakati huu taifa la Jamhuri ya Afrika ya Kati limeanza tena kushuhudia vurugu za kkabila na kidini, machafuko ambayo yamewastua watu walio wengi.

"Ufaransa haiwezi kuitenga Jamhuri ya Afrika ya Kati," amesema Jean-Marc Ayrault waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, wakati alipofanya mahojiano kuelezea hali ya mambo ilivyo nchini humo, ambako kuna vikosi vya wanajeshi takribani elfu 1 wa umoja wa Mataifa wanaolinda amani, chini ya mwavuli wa MINUSCA.

Hata hivyo wananchi wengi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wameeleza wasiwasi wao kufuatia uamuzi huu wa Ufaransa kuanza kuwandoa wanajeshi wake, ambao walipelekwa nchini humo kwa dharura mwezi December mwaka 2013 baada ya machafuko kuzidi.

Mmoja wa wanasiasa wa karibu na rais wa nchi hiyo, akizungumza na shirika la habari la AFP, amesema kuwa makundi ya wapiganaji yameanza kujikusanya na kujiweka tayari, na muda wowote yataanza kutekeleza mashambulizi baada ya vikosi vya Ufaransa kuondoka.

Wanasiasa hao wanasema hali inazidi kuogofya kadiri siku zinavyozidi kwenda ambapo wameiomba Jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kinachoshuhudiwa nchini humo.

Ijumaa ya wiki iliyopita, watu zaidi ya 25 wameripotiwa kuuawa, sita kati yao wakiwa ni wanajeshi wa Serikali, baada ya kuzuka makabiliano kwenye mji wa Bambari ambako walizunguka pia kambi ya vikosi vya MINUSCA.

Makundi ya wapiganaji yameendelea kuenea nchini humo kutokana na taifa hilo kutokuwa na Serikali imara, ambapo waasi kutoka kundi la kiislamu la Seleka wamekuwa wakikabiliana na waasi wa kundi la Kikristo la Anti-Balaka.