NIGERIA-UBAKAJI-SHERIA

Buhari aamuru uchunguzi ufanyike kuhusu tuhuma za ubakaji

Rais wa Nigeria ameamuru uchunguzi kuhusu madai ya unyanyasaji wa kijinsia katika makambi yaliyojengwa kwa minajili ya kuwapokea watu waliokimbia machafuko yaliyokuwa yakitekelezwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram.

Rais wa Nogeria, Muhammadu Buhari asema kusononeshwa na ripoti ya Humana right Watch kuhusu tuhuma za ubakaji zinazowakabili askari wake.
Rais wa Nogeria, Muhammadu Buhari asema kusononeshwa na ripoti ya Humana right Watch kuhusu tuhuma za ubakaji zinazowakabili askari wake. REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa Ofisi ya rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari "alishtushwa" na ripoti ya shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) ambalo linawashtumu maafisa wa vikosi vya usalama vya nchi yake kuwabaka wanawake katika makambi hayo ya wakimbizi.

Rais Muhammadu Buhari ameitaka polisi na Wakuu wa majimbo husika kuanza mara moja uchunguzi ili kutoa mwanga juu ya madai ya HRW.

Kwa mujibu wa Human Right Watch, wanawake 43 walibakwa au kutumiwa kingono na maafisa wa usalama na makundi ya wanamgambo.

Vitendo hivi vya ubakaji vilifanyika katika makambi yaliyojengwa hasa katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi, kwa minajili ya kuwapokea watu waliolazimika kukimbia mauaji yaliyokua yakitekelezwa na wanamgambo wa Boko Haram.

Baadhi ya wanawake waliokuwa wakiishi katika makambi wamesema walilazimishwa kufanya ngono na kutelekezwa wakati walipata ujauzito, kwa mujibu wa Human Rights Watch.

Machafuko yanayoendeshwa na kundi la kijihadi nchini Nigeria yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na watu zaidi ya milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao.